Ijumaa, 23 Mei 2014

FAMILIA YAMWACHIA MUNGU KIFO CHA MENEJA WA EWURA KUFUATIA UTATA ULIOGUBIKA


Mwili wa Gashaza ulitarajiwa kuwasili kijiji cha Mulukulazo wilayani Ngara Mkoani Kagera jana jioni na leo saa 4:00 asubuhi utapelekwa katika Kanisa la Anglikana katika kijiji hicho kwa ajili ya sala na saa 6:00 mchana utaagwa kabla ya mazishi yatakayofanyika nyumbani kwake.

Aliyekuwa Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza anazikwa leo katika Kijiji cha Mulukulazo, Ngara mkoani Kagera huku familia yake ikisema haina cha kusema kuhusu kifo hicho, bali inamwachia Mungu.

Akizungumza jana kijijini hapo, mdogo wa marehemu, Alex Gashaza alisema familia imepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa na kushangazwa na taarifa kwamba ulitokana na kujinyonga kama inavyodaiwa.


Alisema baada ya kupokea simu kutoka Dar es Salaam kuhusu mazingira ya kifo hicho, wameshindwa kujua sababu za kifo kwa kuwa hakuna mtu aliyezungumza naye.


Alisema kaka yake hakuwa na tatizo lolote na wanafamilia, ndugu wala jamaa zake wa karibu, hivyo familia haiwezi kuelezea jambo ambalo halina ushahidi, badala yake inaacha tukio hilo mikononi mwa Mungu.


“Tumekuwa tukishirikiana naye kuendeleza familia yetu, kama unavyoona nyumba ilipokuwa imefikia hatua ya kuezekwa, kuna mchango wake mkubwa kifamilia,” alisema Alex.


Mwili wa Gashaza ulitarajiwa kuwasili Mulukulazo jana jioni na leo saa 4:00 asubuhi utapelekwa katika Kanisa la Anglikana katika kijiji hicho kwa ajili ya sala na saa 6:00 mchana utaagwa kabla ya mazishi yatakayofanyika nyumbani kwake.


Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza mkoani Mwanza, Mchungaji Lazaro Manjelenga ambaye pia ni baba mkwe wa mdogo wa marehemu, alisema wana matumaini na Muumba kwa kile kilichotokea.


“Siri ya Mungu na mwanadamu wake hakuna wa kuijua, hivyo tusihukumu,” alisema na kuongeza kuwa mazishi yatafanyika kwa mujibu wa taratibu za Kanisa hilo.MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni