Kumetokea shambulizi la bomu mbele ya soko lenye shughuli
nyingi katika mji mkuu wa Nigeria Abuja na kuwauwa zaidi ya watu 21.
Taswira ya majonzi na kilio ilitanda katika mji wa Abuja, mamia ya watu
waliokuwa wakinunua bidhaa katika soko hilo wakijikuta wakivuja damu kutokana na
majeraha ya mlipuko huo na wengine kuishia mauti.Walioshuhudia walisema sehemu za miili ya wanadamu zilitapakaa kila mahali sakafuni.
Magari yaliungua kabisa na vioo katika madirisha ya nyumba zilizokuwa karibu kuvunjika vyote. Watu waliokuwa na hofu walielekea kwenye mahospitali yaliyo karibu ambapo walishuhudia magari ya wagonjwa yakisongamana kila mahali yakiwaleta wagonjwa na miili ya waliokufa.
John Tobi Wojioa aliwasili mahali hapo muda mfupi baadaye akimtafuta jamaa wake. Alitaja alichoona kama mafuriko ya damu:
"Kulikuwepo magari ya wagonjwa wa shirika la FRCS (Federal Road Safety Corps) na ya mashirika mengine yaliyokuwa yakiingia na kuondoka yakibeba miili ya waathirika. Kwenye barabara alama za damu za nyayo za wanadamu zilionekana kila mahali," alisema Bwana Wojioa.
Bahati kwa Bwana Wojioa ni kuwa jamaa wake baadaye alipatikana akiwa hai huku akiendelea kutulia kutokana na mlipuko huo.
Hii ni mara ya tatu kwa mji mkuu kulengwa na milipuko tangu Aprili. Kundi la Waislamu wenye itikadi kali la Boko Haramu lilidai kuhusika katika milipuko miwili ya awali ambako zaidi ya watu 90 walifariki.
Milipuko hiyo ilitokea kando mwa jiji lakini huu wa sasa umetokea katikati mwa jiji katika Wilaya ya Wuse 2 na hofu yake itatanda katika mji wote.
Kwa mara nyingine tena Boko Haram watashukiwa kuhusika katika mlipuko huu. Kundi hilo limelipua miji kadhaa nchini Nigeria huku likiendesha kampeni yake ya kuwashambulia raia katika maeneo ya mashambani hasa Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo.
Mnamo Jumanne watu waliokuwa wakitoroka vijiji katika jimbo la Borno walisema kuwa makumi ya wanawake na watoto walikuwa wametekwa nyara.
Lakini Serikali kwa upande wake ikasema kuwa hakuna ushahidi kuwa utekaji nyara ulitendeka.
Serikali ilisema vivyo hivyo wakati zaidi ya wasichana wanafunzi zaidi ya 200 walitekwa nyara na Boko Haram mnamo Aprili.
Wachunguzi wengi wanasema kuwa kwa kukanusha kuwa kuna utovu wa usalama nchini Nigeria, Serikali imechanganyikiwa kwa sababu milipuko ya mabomu ya mara kwa mara ni ushahidi tosha kuwa ukosefu wa usalama ndio ukweli wa mambo nchini (TK)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni