Jumanne, 15 Julai 2014

ALIYEKUWA MKURUGENZI MKUU WA TPA NA MSADIZI WAKE WAPANDISHWA KIZIMBANI



Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Msaidizi wake, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka.

Washitakiwa hao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe pamoja na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, Hamad Koshuma.

Walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincolin akisaidiana na Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekoma.


Wakili Lincolin alidai kuwa Desemba 5 mwaka 2011 katika ofisi ya Mamlaka ya Bandari, washitakiwa wakiwa waajiriwa wa mamlaka hiyo, walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mkataba na Kampuni ya China Communication Contraction.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao, walisaini mkataba huo kwa ajili ya ujenzi wa Geti Namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam, bila kutangaza zabuni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na lilikuwa na lengo la kuinufaisha kampuni ya China.

Washitakiwa walikana kutenda makosa hayo na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kusaini hati ya Sh milioni mbili pamoja na kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni mbili.

Upande wa mashitaka ulidai upelelezi bado haujakamilika. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 13 mwaka huu, itakapotajwa tena.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni