Papa Francis.
MAJONZI yameanza kuwakuta baadhi ya waumini wa kanisa katoliki Bongo kufuatia kiongozi wao wa dunia, Papa Francis (77) kuweka hadharani hatima ya maisha yake. Katikati ya wiki hii, Papa Francis akiwa anarejea Vatican kutoka ziarani Korea Kusini alisema anaamini ana miaka miwili au mitatu ya kuishi duniani na si vinginevyo.
“Najaribu kufikiria kuhusu dhambi zangu na makosa yangu, siwezi kujivuna. Najua kwa sababu hali hii itadumu kwa muda mchache. Miaka miwili au mitatu nitakuwa nimeondoka na kwenda nyumbani kwa baba,” alisema papa huyo kauli iliyozua sintofahamu duniani.
Wachambuzi wa masuala ya kiimani kwa nyakati tofauti walisema huenda kiongozi huyo ana tatizo la kiafya ambalo halijawekwa wazi.
Jijini Dar es Salaam, baadhi ya waumini wa kanisa katoliki waliozungumza na gazeti hili walisema kauli hiyo ya papa imewatia majonzi kwani inawapa tafsiri ya kumkosa siku si nyingi. Samuel Msokali, anaabudu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maxmillian Kolbe, Mwenge yeye alisema:
“Nimepokea kwa majonzi makubwa kauli ile ya papa. Kama anaumwa atuweke wazi waumini wake. Kama amepewa maono na Mungu pia atuweke wazi tujue.”
Mama Juliana, yeye anaabudu Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alisema:
“Siamini kama kweli papa alisema yale maneno. Ni makali sana na yanachoma, nilitoa machozi niliposikia, nimeanza kulia hata kabla siku yake haijafika.”
Muumini mwingine anayeabudu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Anuarite, Makuburi (aliomba jina lake lisiandikwe) alisema anaamini papa ameona katika maono kifo chake kwa sababu ya usafi wa moyo.
“Mimi naamini papa ni msafi wa moyo kwa hiyo ameoneshwa na Mungu kwamba muda wake wa kumtumikia duniani umeisha. Kule kusema ni kutuweka tayari kupokea taarifa,” alisema muumini huyo wa kiume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni