Jumatatu, 1 Septemba 2014

HAKUNA MAPINDUZI LESOTHO - JESHI


Jeshi la Lesotho limekana madai ya kufanya njama ya mapinduzi
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amefanya mkutano wa dharura na waziri mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane, kufuatia taarifa za jaribio la mapinduzi.
Kuna taarifa ya kuwepo pengo la kiongozi katika ufalme huo mdogo wa Lesotho. Haijulikani nani anaongoza nchi hiyo kwa sasa.
 
Jeshi lilizingira makao ya waziri mkuu mapema Jumamosi na kumlazimu kukimbilia nchini Afrika Kusini pamoja na mawaziri wake. Alisema kuwa anahofia maisha yake.
Serikali ya Afrika Kusini ambako waziri mkuu huyo amepata hifadhi, imesema haitastahamili mapinduzi kufanyika katika nchi hiyo.
Inaonekana kulikuwa na njama ya mapinduzi nchini humo, lakini jeshi linasema kila kitu kiko shwari. Baadhi ya viongozi wa kanda hiyo, wanakutana kujadili hatua watakazochukua.
Mkutano wa dharura kati ya Rais wa Afrika Kusini na waziri mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane, ulifanyika Jumapili usiku.
Mkutano huo ulilenga kutafuta nyenzo za kumaliza mgogoro wa kisiasa katika ufalme huo mdogo.
Hali ya taharuki iliibuka Jumamosi jeshi lilipozingira makao makuu ya ulinzi na ikulu ya Rais na kutokea makabiliano kati ya jeshi na polisi. Inaarifiwa kuwa jeshi lilikuwa linamzuia waziri mkuu kumfuta kazi mkuu wa majeshi.
Lakini jeshi limekanusha madai hayo likisema lilipokea taarifa kuwa polisi walikuwa wanapanga kuhami vikundi vya vijana ambao wangefanya maandamano kulazimisha waziri mkuu kufungua vikao vya bunge. Maandamano hayo sasa yamesitishwa.
Waziri mkuu Thomas Thabane, aliingia nchini Afrika Kusini Jumamosi asubuhi na kusema kuwa jeshi lilikuwa linapanga mapinduzi.
Mawaziri wa ulinzi na mambo ya nje wa Namibia na Zimbabwe walishiriki kwenye mkutano huo ingawa taarifa za kilichojadiliwa kwenye mkutano huo bado hazijatolewa (TK).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni