Mbunge wa
Same Mashariki, Anne Kilango Malecela akizozana na dereva wa mkuu wa
wilaya ya Mbozi (aliyekataa kutaja jina lake) baada ya kukuta gari la
mkuu huyo wa wilaya likipeperusha bendera katika jimbo la Same Mashariki
jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Katika
hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Dk Michael
Kadege limekutwa likipeperusha bendera katika eneo la Wilaya ya Same
mkoani Kilimanjaro na kuzua tafrani kati ya mkuu huyo na Mbunge wa Same
Mashariki, Anne Kilango Malecela.
Gari hilo
likiwa na Bendera, lilionekana saa nne asubuhi likiwa
limeegeshwa katika eneo la Mamba Myamba katika Jimbo la Same Mashariki
huku Dk Kadege akiwa kwenye mgahawa.
Kitendo cha gari hilo kuonekana likipeperusha
bendera kilimfanya Kilango kulifuata akidhani ni la Mkuu wa Wilaya ya Same, ndipo akakuta ni la Mbozi.
“Hili
gari siyo la Same na kawaida mkuu wa wilaya nyingine haruhusiwi
kupeperusha bendera kwenye eneo ambalo siyo lake, huyu amekuja kwenye
mambo yake ya siasa, anapeperusha bendera ili wananchi wamwone kuwa yuko
juu na hii ni hujuma kwenye jimbo langu,” alilalamika Kilango.
Alisema
Dk Kadege ni miongoni mwa watu wanaotaka kugombea ubunge Jimbo la Same
Mashariki lakini ni vyema akasubiri muda ukifika ajitokeze hadharani
badala ya kujenga mpasuko kwa CCM katika jimbo hilo.
“Huyu
amekuja kwa ajili ya vikao vya ndani, mwaka 2005 tuligombea wote kwenye
kura za maoni nikamshinda nikiwa na kura 389 yeye 46 akawa mtu wa nne,
mwaka 2010 mimi nilipata kura 7,900 na yeye alipata 2,200 sasa ameanza,
sikatai lakini asubiri muda wake,” alisema Kilango.
Kwa
upande wake, Dk Michael Kadege alisema hakuwa na taarifa kuwa gari lake
linapeperusha bendera kwa kuwa yeye hahusiki kuweka bendera, akataka
dereva wake aeleze sababu za kupeperusha bendera kwenye eneo
lisiloruhusiwa.
Dk Kadege
alisema yeye yuko likizo na alikwenda nyumbani kwao Same kupumzika na
hafanyi shughuli zozote za kisiasa katika jimbo hilo kama inavyodaiwa na
Kilango.
Dereva wa
mkuu huyo wa wilaya ambaye alikataa kutaja jina lake, alipohojiwa
sababu za kupeperusha bendera katika eneo lisiloruhusiwa alisema alikuwa
akifanya usafi wa gari na alipohojiwa zaidi alidai siyo msemaji wa mkuu
wa wilaya.
Mkuu wa
Wilaya ya Same, Herman Kapufi alisema kutokana na sheria, utaratibu na
miongozo ya wakuu wa wilaya, kiongozi huyo wa wilaya haruhusiwi
kupeperusha bendera katika eneo ambalo siyo lake.
Alisema
kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa namba 19 ya Mwaka 1997 na Sheria
ya Serikali za Mitaa namba Saba na Nane ya mwaka 1982, mkuu wa wilaya
ni msimamizi wa shughuli za kimaendeleo na mwenyekiti wa kamati ya
ulinzi na usalama katika wilaya yake tu.
Kapufi
alisema atawasiliana na Dk Kadege kama anafahamu utaratibu na miongozo
waliyopewa wakati wa kuanza kazi ili ajue kama alikusudia kufanya hivyo
au kama alipitiwa.
Mwenyekiti
wa CCM Wilaya ya Same, Agust Kessy alipoulizwa kuhusu hali hiyo alisema
mipaka ya wakuu wa wilaya inatambulika ni jambo la kushangaza kama mkuu
huyo alikuwa ndani ya gari na asiione bendera ikipepea.
Alisema
CCM imeweka utaratibu na kanuni zinazotakiwa kufuatwa na kila mwanachama
na kuwataka wenye lengo la kugombea wasubiri muda ufike ili kuepusha
mgongano na mtafaruku ndani ya chama. “Tuache kutegeana, tusubiri
filimbi ipigwe,” alisema Kessy.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni