Mwanamgambo anayejulikana kwa jina la utani 'Jihadi John' wa kundi la
wanamgambo wenye itikadi kali la dola la kiislamu IS, ambaye amekuwa
akionekana katika video akiwachinja mateka ametambuliwa kama Mohammed
Emwazi
Mohammed Emwazi ni raia wa Uingereza, mtaalamu wa masuala ya programu za
kompyuta anayetokea familia inayojiweza iliyoko mjini London na alikuwa
akifahamika na maafisa wa usalama nchini Uingereza hata kabla ya
kuelekea Syria.Mwanamgambo huyo ambaye huonekana katika video za kundi la IS akiwa amevalia nguo nyeusi na kuufunika uso wake, kushikilia kisu na kuzungumza kizunguchenye lafudhi ya Kiingereza anaaminika kuwa mchinjaji wa mateka wa kundi hilo wakiwemo raia wa Marekani, Uingereza na Syria.
'Jihadi John' kama anavyojulikana kwa jina la utani kutokana na lafudhi yake ya kiingereza ana umri wa miaka 26 na alitumia video hizo kutoa vitisho kwa nchi za magharibi na viongozi wake wakiwemo Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kabla ya kuwatisha mateka ambao huwa wamevalishwa magwanda ya rangi ya chungwa.
Emwazi ni mzaliwa wa Kuwait
Emwazi amefichuliwa kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari vya Uingereza ambavyo vimeripoti alizaliwa Kuwait na alikwenda Uingereza na familia yake akiwa na umri wa miaka sita.
Alihitimu na digrii ya masuala ya kompyuta kutoka chuo kikuu cha Westminister na shirika la ujasusi la Uingereza MI5 lilianza kufuatilia nyendo zake. Hayo ni kulingana na mkurugenzi wa shirika la utafiti la Cage linalowatetea watuhumiwa wanaozuiwa kwa mashitaka ya ugaidi Asim Qureshi.
Qureshi amesema shirika hilo la ujasusi lilijaribu mara kadhaa kumsajili Emwazi kujiunga nalo na baadaye kumzuia kusafiri nje ya Uingereza na hivyo kumlazimu kutoroka bila ya kuiarifu familia yake. Inaaminika mwanamgambo huyo alisafiri kuelekea Syria mwaka 2012.
Serikali ya Uingereza imekataa kuzungumzia ufichuzi huo kumhusu jihadi John na kusema uchunguzi bado unaendelea.
Mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza yametumia mbinu kadhaa za uchunguzi zikwemo za kutambua sauti na sura pamoja na kuwahoji mateka walioachiwa huru na IS kumtambua mwanamgambo huyo.
Shirika la Cage limedai Emwazi alihisi mfungwa kwa kuandamwa na maafisa wa kijasusi. Inadaiwa Emwazi alizuiwa nchini Tanzania mwezi Agosti mwaka 2009 alipokwenda kwa safari ya kitalii na marafiki zake wawili.
Huku hayo yakijiri, nchini Iraq wanamgambo wa IS wameharibu sanamu za kale za thamani kubwa ambayo ni sehemu ya turathi ya nchi hiyo katika mji wa Mosul.
IS yaharibu vito vya thamani Iraq
Uharibifu huo umeibua shutuma kali kutoka kwa wataalamu wa turathi na wanaikolojia walioufananisha na ule uliofanywa na kundi la Taliban nchini Afghanistan mwaka 2001.
Shirika la umoja wa Mataifa la tamaduni na turathi limetaka kuitishwa mkutano wa dharura wa baraza la usalama la umoja huo kujadili uharibifu huo ambao limeutaja sehemu muhimu ya usalama wa Iraq.
Hayo yanakuja huku hofu ikitanda nchini Iraq na Syria baada ya kuripotiwa kuwa wanamgambo hao wamewateka nyara zaidi ya wakristo 220 katika kipindi cha siku tatu zilizopita.
Marekani na washirika wake zimefanya mashambulizi kumi na nne katika nchi hizo mbili tangu Jumatano asubuhi dhidi ya ngome za IS
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni