Unatimu mwaka wa 70 tokea majeshi ya nchi yaliyofungamana dhidi ya
fashisti Hitler kuushambulia kwa ndege mji wa Dresden, mashariki mwa
Ujerumani. Maalfu ya watu walikufa kutokana na mashambulio hayo.
Habari juu ya idadi ya vifo zinatafautiana. Baadhi wanasema watu 70,000
walikufa, wengine wanasema watu 35,000 waliuawa na wengine wanasema
waliouawa walikuwa 25,000 kutokana na mashambulio ya ndege yaliyofanywa
tarahe 13,14 na 15 mwezi February 1945 katika mji huo wa Dresden.Mwanzo wa mashambulio
Mashambulio ya mji huo yalianza tarehe 13/2. Ndege 245 aina ya Lancaster ziliruka kutokea Uingereza kuelekea mji wa Dresden. Wakati huo mji huo ulikuwa na wakaazi 630,000 na maelfu ya wakimbizi. Lakini mji huo haukuwa na umuhimu kijeshi wala kiuchumi hata kidogo. Hata hivyo hatima ya vita ilikuwa tayari imeshajulikana mnamo mwaka wa 1944. Majira ya saa tatu na dakika 39 usiku, ving'ora vilisikika katika mji wa Dresden.
Maelfu kwa maelfu ya mabomu yalidondoshwa katika mji huo uliokuwa maarufu kutokana na majengo yake mazuri na tunu zake za kitamaduni.
Mji uliwaka moto. Katika muda mfupi wa dakika 23 mji huo uliwaka moto kiasi kwamba marubani wa Uingereza waliripoti kutokea umbali wa kilometa zaidi ya mia tatu kwamba mji huo ulikuwa unawaka moto.
Marubani waliweza kuuona mji ukiungua kutokea angani umbali wa mita 6700. Joto lilikuwa kubwa la kuyeyusha kioo. Eneo la kilometa 15 za mraba liliteketezwa na mabomu yaliyodondoshwa na ndege za Ungereza na kufuatia baadae na ndege za Marekani.
Sir Arthur ndiye aliesimamia mashambulizi
Mamia kwa mamia ya marubani wa Uingereza na Marekani walishiriki katika mashambulio ya kuuteketeza mji wa Dresden, lakini ni mtu mmoja tu aliyekuwa msimamizi, Arthur Harris, aliyekuwa mkuu wa kikosi cha anga cha Uingereza Royal Air Force. Alikuwa mtekelezaji mkuu wa mpango wa Waziri Mkuu Winston Churchil wa kuishambulia Ujerumani ya mafashisti, yaani mkakati wa kuwavunja ari kabisa maadui.
Kwa nini mji wa Dresden ulishambuliwa?
Baadhi ya wataalamu wa historia walitathmini kushambuliwa kwa mji wa Dresden kuwa ni sehemu ya kuimarishwa uhusiano wa kijeshi baina ya nchi za magharibi na Umoja wa Kisoviet. Mashambulio ya nchi za magharibi dhidi ya Ujerumani ya Hitler yalikuwa yamekwama, katika upande wa magharibi, wakati majeshi ya Umoja wa Kisoviet yalipokuwa yanasonga mbele kwa kasi kubwa , katika upande wa mashariki.
Palikuwapo na mawazo juu ya kuishambulia miji mingine kama Berlin.Lakini mkuu wa kikosi cha anga cha Uingereza, Royal Air Force, Harris aliyaekeleza macho yake katika mji wa Dresden. Nchi zilizofungama kijeshi dhidi ya Hitler ziliuona mji wa Dresden kuwa na uwezekano mkubwa wa kugeuka maficho ya fashisti Adolf Hitler na manazi wengine.
Jemadari Shukov wa Umoja wa Kisoviet na majeshi yake alikuwapo umbali wa kilometa 80 tu kutoka mji wa Dresden,wakati ndege za Uingereza na za Marekani zilipokuwa zinaupiga mabomu mji huo.
Suala la utatanishi: Mpaka leo mashambulio hayo ni suala la utatanishi kihisia pia nchini Uingereza kwenyewe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni