Zitto: Iko siku nitashika nafasi kubwa Tanzania
Na Antony Kayanda na Saumu Mwalimu, Mwananchi
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
amesema kutimuliwa uanachama na Chadema ni dhoruba inayomkumba
mwanasiasa yeyote anayefanikiwa na kwamba iko siku atashika “nafasi
kubwa ya uongozi ya kuwatumikia Watanzania”.
Zitto aliwasili mjini hapa juzi, ikiwa ni siku
chache baada ya Chadema kutangaza kumtimua uanachama kwa kosa la
kupeleka mgogoro wa ndani ya chama kwenye mahakama.
Alifungua kesi Mahakama Kuu akitaka imuamuru
katibu mkuu wa Chadema kumpa nyaraka za mwenendo wa vikao vya Kamati Kuu
vilivyomvua madaraka yote na baadaye kukizuia chama hicho kumjadili.
Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali shauri lake na Chadema ikatangaza
mara moja kumtimua.
Akihutubia mamia ya watu kwenye Kijiji cha
Nyarubanda ambako alikabidhi gari la wagonjwa, Zitto aliwatoa hofu
wananchi hao walioonyesha shauku ya kujua hatma yake na kuwaeleza kuwa
hajawatupa, ataendelea kuwahudumia.
“Hakuna kiongozi aliyefanikiwa kisiasa bila
kupitia misukosuko ya kupingwa,” alisema Zitto ambaye anamalizia kipindi
cha pili cha ubunge wake kwenye jimbo hilo.
“Waziri Mkuu za zamani ya India, Indira Gandhi
alifukuzwa na chama chake na aliamua kuunda chama kipya na baadaye
kuwashinda waliomfukuza katika uchaguzi. Kwa hiyo nawatoa hofu kwa maana
ninajengwa zaidi kisiasa.
“Nipo kwenye dhoruba ambayo inanijenga kisiasa na
ipo siku nitawatumikia Watanzania katika nyadhifa kubwa za uongozi.”
Katika mkutano huo ambao wananchi walimpokea wakiwa na mabango yenye
ujumbe mbalimbali kama “Mheshimiwa Zitto tulikuchagua wewe na siyo
chama,” huku mengine yakiandikwa “chama siyo bora, ubora ni utendaji
kazi”.
Viongozi mbalimbali wa CCM na vyama vingine vya
siasa walijumuika kwenye uwanja huo kumpokea Zitto na kushiriki naye
kucheza ngoma za asili.
Baadhi ya viongozi hao ni mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Hamisi Betese, mkurugenzi wa halmashari
hiyo, Michael Mwandezi na viongozi wengine wa serikali za mitaa.
Akiongea katika hadhara hiyo, Betese alisema kuwa
kitendo cha Zitto kutoa gari ambayo aliwaahidi wananchi kipindi cha
uchaguzi ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo ndiyo chama tawala.
Aliongeza kuwa yeye kama mwenyekiti wa halmashauri
bado anamtambua Zitto kama mbunge wa Kigoma Kaskazini mpaka hapo
taarifa rasmi zitakapotolewa.
Wanakijiji hao walishukuru Zitto kwa kutoa gari
hilo wakisema litawasaidia kuokoa fedha nyingi walizokuwa wakitumia
kutafuta magari binafsi wanapokuwa na wagonjwa wanaohitaji matibabu ya
haraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni