Jumamosi, 18 Aprili 2015

HATUSOGEZI UCHAGUZI MKUU MBELE : NEC

Tume ya taifa ya uchaguzi NEC imesema haina mpango wa kusogeza mbele uchaguzi mkuu wa rais na wabunge kutokana na uwezekano wa kutokamilika kwa daftari la kudumu la wapiga kura. Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Damian Lubuva amesema hayo jijini Dar es Salaam ambapo amesema Tume imepokea mashine za BVR 248 na kufanya jumla ya mashine hizo kufikia 498 na kuongeza kuwa muda mfupi ujao watapokea nyingine 1600 zinazowasili kwa ndege ya kukodi kutoka Dubai.
Aidha jaji Lubuva ametaja awamu ya pili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura itaendelea April 24 mwaka huu, siku ambayo pia watapokea BVR nyingine 1600 ambazo amesema zitaharakisha kasi ya uandikishaji kwani wataweza kuandikisha mikoa mingi kwa wakati mmoja na kuongeza kuwa awamu ya pili ya zoezi la BVR itakuwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kitengo cha daftari la wapiga kura Sisti Karia amesema endapo wangekuwa na mashine za BVR za kutosha wangezigawa kwenye halmashauri nchi nzima hivyo wangeweza kuendesha zoezi la kuandikisha watu kwa siku 28 tu nchi nzima

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni