Jumatano, 22 Aprili 2015

SAUDIA YASIMAMISHA MASHAMBULIZI DHIDI YA WAHOUTHI YEMEN

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umetangaza kumalizika kwa operesheni ya anga dhidi ya wahouthi nchini Yemen, na kuingia katika mchakato wa kisiasa. Iran na Marekani zimesema uamuzi huo ni hatua nzuri.
Mashambulizi ya anga dhid ya wahouthi yamekuwa yakiendelea kwa wiki nne Mashambulizi ya anga dhid ya wahouthi yamekuwa yakiendelea kwa wiki nne
Muungano huo umesema umefikia uamuzi wa kusimamisha mashambulizi hayo ya anga ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki nne sasa, baada ya kutimiza malengo yake ya kijeshi, ya kuondoa kitisho cha usalama wa Saudi Arabia na nchi nyingine majirani.
Umesema sasa unageukia mchakato wa kisiasa kujaribu kuusuluhisha mgogoro wa Yemen, na kuongeza kuwa uwezekano wa kuanza upya kwa mashambulizi hayo unaachwa wazi, ikiwa hali italazimu hivyo. Vile vile, kulingana na tangazo la muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia, mzingiri wa bahari na anga utaendelea dhidi ya Yemen, ambayo iko katika eneo la kimkakati katika Mashariki ya Kati.
Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia Brigedia Jenerali Ahmed Asiri amesema uamuzi huo umefuatia ombi la rais wa Yemen. Abd-Rabo Mansour Hadi aliyeko ukimbizini nchini Saudi Arabia.
Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia, Brigedia Jenerali Ahmed Asiri Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia, Brigedia Jenerali Ahmed Asiri
Amesema, ''Leo uongozi wa muungano umeamua kusimamisha operesheni ''Dhoruba Kabambe'' kufuatia maombi ya rais wa Yemen, ambaye anaamini malengo makuu ya operesheni hiyo yametimia, kitisho kwa watu wa Yemen kimeondolewa, na waasi wa kihouthi wamepoteza uwezo wa kuwatisha watu wa Yemen na jirani zao. Serikali ya Yemen itachukua hatua kuwarejeshea matumaini watu wa nchi hiyo''.
Bado wahouthi wanashika hatamu
Hata hivyo licha ya madai hayo ya mafanikio, waasi wa kihouthi bado wanaudhibiti mjini mkuu wa Yemen, Sanaa, na rais Abd-Rabo Mansour Hadi bado yuko ukimbizini nchini Saudi Arabia. Hali kadhalika mapambano makali yanaendelea katika mji wa bandari wa Aden.
Iran, taifa la kishia ambalo linashutumiwa kuwaunga mkono wahouthi, imeukaribisha uamuzi huo wa kusitisha mashambulizi, ikisema ni hatua nzuri inayofungua mlango kwa njia za kisiasa kuusuluhisha mzozo wa Yemen.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema hatua hiyo haina budi kufuatiwa na msaada wa kibinadamu na mjadala miongoni mwa wayemen na serikali yenye kushirikisha makundi yetu. ''Tuko tayari kusaidia'', amesema waziri huyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
Marekani yapeleka meli za kivita
Marekani yajizatiti kuweza kuizuia Iran kupeleka silaha Yemen
Marekani yajizatiti kuweza kuizuia Iran kupeleka silaha Yemen
Marekani pia imesema imelipokea vyema tangazo hilo la kusimamisha mashambulizi dhidi ya wahouthi, na kutoa rai ya kufanyika haraka mazungumzo ili kuepusha mvutano baina ya mataifa yenye ushawishi katika ukanda huo.
Hata hivyo Marekani imetuma meli yake ya kubeba ndege za kivita USS Theodore Roosevelt, ikisindikizwa na nyingine ya kubeba makombora USS Normandy, kukiwa na ripoti kwamba msafara wa meli tisa za Iran zimeng'oa nanga na kuanza safari baharini.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Kanali Steven Warren amesema meli za Marekani zilikuwa zikijiandaa kuuzuia msafara huo wa Iran, ikiwa utakuwa umebeba silaha.
Waasi wa kihouthi wameitisha maandamano makubwa mjini Sanaa leo, kuadhimishwa kusitishwa kwa mashambulizi ya Saudi Arabia na washirka wake.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni