Ijumaa, 17 Aprili 2015

UJERUMANI YAFANYA IBADA KUWAKUMBUKA WALIOKUFA AJALI YA GERMANWINGS

Ujerumani inafanya ibada maalum kuomboleza vifo vya watu 150 waliopoteza maisha yao katika ajali ya ndege ya Germanwings inayoaminika kuangushwa kwa makusudi na msaidizi wa rubani katika milima ya Ufaransa mwezi uliopita
Bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kote nchini Ujerumani hii leo huku viongozi wa kisiasa na kidini wakijumuika na mamia ya jamaa za waathiriwa leo mchana kwa ibada ya makumbusho ya wafu itakayofanyika katika kanisa kuu la Cologne.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck watawaongoza viongozi wengine wa kisiasa katika kuhudhuria misa hiyo inayoyaleta pamoja madhehebu mbali mbali. Waziri wa mambo ya ndani wa Uhispania Jorge Fernendez Diaz na waziri wa uchukuzi wa Ufaransa Alain Vidalies pia wanahudhuria misa hiyo.
Maua na mishumaa kuwakumbuka waathiriwa
Takriban wageni 1,500 wakiwemo jamaa 500 wa waathiriwa wa ajali hiyo ya ndege ya Germanwings wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo itakayoonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya Ujerumani.
Wachunguzi katika milima ya Ufaransa wakitafuta mabaki ya ndege ya Germanwings Wachunguzi katika milima ya Ufaransa wakitafuta mabaki ya ndege ya Germanwings
Waombolezaji wanaruhusiwa kuacha maua na mishumaa katika ngazi za kanisa hilo la Cologne na nje ya kituo kikuu cha reli cha mji huo kilicho karibu na kanisa hilo. Mishumaa 150 itakayowakilisha watu wote waliokuwa katika ndege hiyo aina ya Airbus chapa A-320 itawashwa mbele ya madhabahu.
Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki la Cologne Kadinali Rainer Maria Woelki na kiongozi mkuu wa kanisa la Protestanti wa Westphalia Annette Kurschus wataiongoza misa hiyo.
Ndege hiyo ya shirika la Germanwings ambalo ni shirika tanzu la Shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa ilikuwa inatoka Barcelona kuelekea Duesseldorf mnamo tarehe 24 mwezi Machi wakati, kulingana na maoni ya wachunguzi, ilipoangushwa kwa makusudi na msaidizi wa rubani Andreas Lubitz aliyekuwa na maradhi ya msongo wa mawazo baada ya kumfungia nje ya chumba cha rubani rubani mkuu.
Ujerumani iliwapoteza raia 72, 16 kati yao wanafunzi wa shule ya upili waliokuwa wakitoka ziarani nchini Uhispania. Raia 50 wa Uhispania pia waliuawa katika ajali hiyo.
Ibada ya kuashiria umoja wa kitaifa
Jamaa za waathiriwa awali walikuwa wamefanya misa nyingine ya makumbusho karibu na eneo la mkasa katika kijiji cha Le Vernet nchini Ufaransa. Mnamo tarehe 13 mwezi huu mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Uhispania na Ufaransa walitoa rambi rambi zao katika uwanja wa ndege wa Barcelona.
Kanisa kuu la Köln kunakofanyika ibada Kanisa kuu la Köln kunakofanyika ibada
Wanasaikolojia wanasema kuja pamoja kwa jamii ya wajerumani kuomboleza na kuwakumbuka waliofariki katika ajali hiyo ni ishara ya umoja wa kitaifa na italeta faraja.
Profesa wa masuala ya saikolojia katika chuo kikuu cha Leipzig Immo Fritsche amesema wajerumani wameungana tangu kufichuliwa kuwa ajali hiyo ilisababishwa na masidizi wa rubani na kisa hicho kinahitaji watu kuwa na hakikisho kuwa kuna haja ya kujizuia kufanya vitendo vitakavyowadhuru wengine na hasa jamii inataka kuwa na hali ya kuamini tena kuwa walio na udhibiti wa vyombo kama ndege wanaweza kutegemewa na wanajali usalama wao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni