Jumatatu, 4 Mei 2015

MBINYO WAZIDI KWA MERKEL JUU YA SAKATA LA UDUKUZI

Washirika wa muungano wa serikali ya Kansela Angela Merkel na wapinzani wanazidi kutoa mbinyo kwa ofisi yake kutoa maelezo juu ya madai ya karibuni dhidi ya shirika la uchunguzi wa nje la Ujerumani BND.
Ralf Stegner, makamu mwenyekiti wa chama cha SPD, ambacho kinaunda serikali ya muungano pamoja na chama cha Kansela Merkel cha Christian Democratic CDU, alitumia mahojiano ya gazetini kuitaka ofisi yake kueleza kila inachokijua kuhusiana na madai hayo.
"Kwa Kansela Merkel, mchezo wa kujitenga na ufichuzi wa karibuni na kusema hayamhusu umekwisha," alisema Stegner katika mahojiano na gazeti la Süddeutsche toleo la Jumatatu.
Alisema hii ina maana kuwa waziri wa sasa anayehusika na masuala ya ofisi ya Kansela Peter Altimaier, pamoja na watangulizi wake wawili Ronald Pofalla na waziri wa sasa wa mambo ya ndani Thomas de Maizere, wanapaswa kufika mbele ya kamati maalumu ya bunge iliyoundwa kutoa mwanga juu ya shughuli za uchunguzi wa shirika la Marekani NSA.

Kituo cha kurekodia mawasiliano cha Bad Aibling kilichopo kusini mwa Ujerumani kinachodaiwa kutumiwa na BND kuifanyia ujasusi NSA. Kituo cha kurekodia mawasiliano cha Bad Aibling kilichopo kusini mwa Ujerumani kinachodaiwa kutumiwa na BND kuifanyia ujasusi NSA.
Watatu hao wote ni wanachama wa chama cha Merkel cha CDU. De Maizere ambaye aliongoza ofisi ya Kansela kati ya mwaka 2005 na 2009, anatarajiwa kuhudhuria mbele ya kamati ya uchunguzi ya bunge siku ya Jumatatu.
Miito kwa Merkel kutoa ushahidi
Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha upinzani bungeni cha Die Linke Gregor Gysi, ametaka Kansela Merkel mwenyewe ahojiwa na kamati inayochunguza shughuli za NSA. Gysi alisema katika mahojiano na shirika la utangazaji la umma ARD siku ya Jumapili, kuwa Markel lazima atoe ushahidi chini ya kiapo. Aliongeza kuwa ni wazi kuwa ofisi ya Kansela ilishindwa katika majukumu yake kama msimamizi wa shughuli za ujasusi.
Sakata hilo limeibua maswali mengi na sasa tume ya uchunguzi ya NSA inataka kufahamu undani wa ushirikiano kati ya NSA na BND. "Tunapaswa kuangalia kwa umakini iwapo ushirikiano wa miaka mingi kati ya NSA na BND umeathiri maslahi ya Ujerumani, na kisha tutahitaji majibu ya nani alijua nini na kwa wakati gani," alisema Patric Sensburg, mwenyekiti wa kamati hiyo.
Madai haya ya sasa yaliripotiwa kwa mara ya kwanza katika toleo la Jumamosi la jarida la kila wiki la Der Spiegel. Lilisema shirika la ujasusi la BND lilifuta maombi 12,000 kutoka NSA, ambayo yalikuwa yanawalenga maafisa kadhaa waandamizi wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, na vilevile maafisa wa taasisi za Umoja wa Ulaya na mataifa kadhaa ya Ulaya.
Kansela Merkel anatakiwa aeleze Kila anachokijua kuhusu shughuli za BND na NSA. Kansela Merkel anatakiwa aeleze Kila anachokijua kuhusu shughuli za BND na NSA.
Fedheha kwa Ujerumani
Kundi la makampuni ya Airbus AIR.PA, lilisema siku ya Alhamisi kuwa linapanga kufungua malalamiko kwa serikali ya Ujerumani, kuhusiana na ripoti kwamba BND iliisaidia NSA kulichunguza pamoja na mashirika mengine ya Ulaya.
Der Spiegel lilisema BND iliisaidia NSA kwa kipindi kisichopungua miaka kumi, na kuifedhehesha Ujerumani na kuwakasirisha wengi katika taifa hili ambako suala la uchunguzi ni nyeti kutokana na ukiukaji wa Wanazi na shirika la ujasusi la Ujerumani Mashariki la Stasi. Ofisi ya Mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani, imetangaza kuanzisha uchunguzi kuhusiana na madai hayo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpd,dw.
Mhariri: Daniel Gakuba

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni