Jumatano, 6 Mei 2015

WANAJESHI WAWILI WA JWTZ WAUAWA DR CONGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amelaani vikali shambulizi la waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambalo limeua wanajeshi wawili wa umoja huo ambao wanatoka Tanzania.
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria Mashariki mwa Kongo Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria Mashariki mwa Kongo
Shambulizi hilo lilifanywa Jumanne jioni katika kijiji cha Kisiki, umbali wa km 38 Kaskazini mwa mji wa Beni. Mbali na wanajeshi wawili waliuawa, 13 walijeruhiwa na wengine wapatao 4 hawajulikani walipo.
Wanajeshi wa Tanzania ambao ni sehemu ya kikosi maalumu cha kuingilia kati walikuwa wakifanya doria walipofanyiwa shambulizi hilo na watu wanaoaminika kuwa waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda.
Umoja wa Mataifa walaani shambulizi hilo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema Katibu Mkuu huyo amesikitishwa sana na shambulizi hilo, na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea na juhudi zake za kuhakikisha usalama wa wakazi wa Mashariki mwa Kongo wanaokabiliwa na vitisho vya waasi.
Shambulizi hilo la jana Jumanne lilikuwa la pili kufanywa dhidi ya Umoja wa Mataifa nchni Kongo katika muda wa saa 48, kwani, siku moja kabla, helikopta iliyokuwa imembeba mkuu wa kijeshi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, ilishambuliwa na watu ambao bado hawajatambuliwa.
Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler amesema hatawendelea kuvumilia mashambulizi hayo ya mara kwa mara dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Beni, na kuongeza kuwa MONUSCO itafanya operesheni kali dhidi ya waasi.
Jeshi la Kongo laishinikiza ADF
Wakazi wa Mashariki mwa Kongo wamekuwa wakisumbuliwa na harakati za waasi kwa miongo miwili Wakazi wa Mashariki mwa Kongo wamekuwa wakisumbuliwa na harakati za waasi kwa miongo miwili
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo liliripoti jana kwamba liliwauwa waasi 16 wa ADF, katika mapambano makali yaliyofanyika eneo hilo mwishoni mwa juma lililopita. Jeshi hilo lilianzisha mwaka jana, operesheni iliyoitwa Sukola, kwa azma ya kuwatokomeza waasi wa ADF ambao wanashutumiwa kuwauwa watu 300 katika vijiji vilivyo karibu na mji wa Beni kati ya mwezi Oktoba na Desemba. Vikosi vya Umoja wa Mataifa vililiunga mkono jeshi la Kongo katika operesheni hiyo.
Eneo la Mashariki mwa Kongo limekuwa likikabiliwa na misukosuko kutokana na makundi mengi ya waasi, ADF ikiwa miongoni mwa makundi hayo, tangu kutokea kwa mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994.
MONUSCO ndio ujumbe mkubwa zaidi wa amani wa Umoja wa Mataifa kwa wakati huu, na unakihusisha kikosi maalumu chenye majukumu ya kipekee ya kuwashambulia waasi. Umoja wa Mataifa umesema kuwa hadi tarehe 31 Machi mwaka huu, waajeshi wake 86 wamekufa nchini Kongo, wengi kutokana na maradhi na ajali.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/ape
Mhariri: Iddi Ssessanga

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni