Jumanne, 30 Juni 2015

MASHUJAA MASHARIKI YA KONGO

Mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kila mkaazi aliwahi wakati mmoja kuwa mkimbizi. Ndio maana mshikamano ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa. Watu wanahiari kukaa na njaa, mradi wanafanikiwa kuwasaidia wageni
Eneo la Rushuturu-Mashariki ya jamhuri ya kidemopkrasi ya Kongo
Baadhi ya wakati Kavuatto Myvayos hutumia mkono wake wa kushoto, kujikanda mgongo ulioanza kupinda. Kazi za shamba zinamshinda hivi sasa bibi huyo, mkongomani mwenye umri wa miaka 60. Anamwangalia Jeannette Masika Kirimbo anayefunga kamba katika konde lake. "Mistari lazima ifuatane vyema, unapopanda njugu," anasema Kirimbo. "Baadaye itakuwa rahisi kutofautisha mmea na magugu," anasema.
Wakulima dazeni moja hivi, wake kwa waume wanamsikiliza Kirimbo. Wanaishi katika eneo la mbali la mashariki ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, si mbali na mji wa Beni. Na ingawa kwa muda mrefu maisha yao yamekuwa wakitegemea kilimo, hivi sasa ndio kwanza wanajifunza kwa msaada wa shirika la Ujerumani la kupambana na njaa duniani - Welthungerhilfe- jinsi ya kuzidisha mavuno kwa wepesi.

Hilo ni jambo muhimu sana katika eneo lao kwa sababu licha ya kuwepo miti na milima inayoleta mandhari ya kuvutia na ya rutuba, lakini kuna vita. Kwa miongo kadhaa sasa makundi ya wanamgambo wanapigana mashariki ya Kongo, ili kudhibiti mali ghafi, ardhi na madaraka. Wananchi wanasumbuliwa, wanaandamwa na mamia kuuliwa. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu milioni mbili na laki sita, wameshayapa kisogo maskani yao.
Ukarimu ni jambo la kawaida Mashariki ya Kongo
Wakimbizi wa ndani katika jamhuri ya kidemkrasi ya Kongo
Wawili kati yao wanaishi tangu miezi kadhaa sasa kwa Kavuatto Myvayo. "Sikuwa na njia nyengine, isipokuwa kuwapokea," anasema bibi huyo ambae ni mkulima. "Walikuwa na shida nisingeweza kuwafukuza." Na hawajampa shida pia watu hao wawili. Baada ya muda kupita ndipo ilipoanza kujulikana kuwa Familia ya Myvayos, walibidi wasamehe chakula kimoja kwa siku tangu walipowakaribisha watu hao.
"Huku,katika eneo hili, ukarimu ni jambo la kawaida," anasema Augustin Kambalo Muyisa. Yeye ni naibu mkurugenzi wa mradi wa shirika la Welthungerhilfe, katika jimbo la Beni. "Zaidi ya hayo, huku takriban kila mtu aliwahi kuwa mkimbizi na kuhitaji kusaidiwa na watu asiowajua. Kwa hivyo kila mmoja anatambua hali ya aina gani wanakabiliana nayo wakimbizi. "Mashariki ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo hakuna kambi za wakimbizi, licha ya mamilioni ya wakongomani walioyapa kisogo maskani yao, bila ya kuwataja maelefu ya warundi na wakimbizi wengine kutoka nchi nyengine jirani.
"Hata kabla ya vita watu walikuwa na kile ambacho ni lazima tu kuwa nacho," anasema Muyisa. Kwamba sasa wanalazimika kuwahudumia pia wageni kwa miezi kadhaa, hakiwezi kutosha. "Matokeo yake ni uhaba wa chakula bora, Muyisa anafika hadi ya kuzungumzia kuhusu "ishara za njaa". Na hasa kwa watoto wadogo, mtu hakawiii kugundua. Baadhi ya mashirika ya misaada katika eneo hilo, yanawasaidia watu katika eneo hilo kuweza kupunguza shida za kiuchumi tangu kwa wahamiaji mpaka kwa wale wanaowakaribisha.
Welthungerhilfe lasaidia Mashariki ya Kongo
Nembo ya shirika la Ujerumani la kupambana na njaa duniani
Na shirika la Ujerumani la kupambana na njaa duniani-Welthungerhilfe, nalo pia kwa miaka sasa limekuwa likiwasaidia wakimbizi na familia zinazowapokea. Kwa makundi hayo mawili na kwa wengineo, shirika hilo limeanza msimu huu kuwapatia mbegu. Wahusika wana nafasi ya kuchagua mbegu tatu. Huko Lume, katika kijiji cha Kavuatto Myavayo, wamechagua kupokea mbegu za njugu, maharagwe na mahindi. Zaidi ya hayo kila familia inapatiwa majembe mawili. Kwa namna hiyo katika eneo la karibu na beni, watu kumi kutoka kila familia moja kati ya 5000 wamepatiwa msaada huo.
Mara nyingi wakimbizi husalia muda mrefu zaidi kuliko vile walivyofikiria. Masika Bahondira amesalia miezi minane. Katika eneo alikozaliwa bibi huyo mwenye umri wa miaka 30, tangu msimu wa mapukutiko uliopita, mauaji ya kikatili yamekuwa yakiripotiwa. Pekee katika kipindi cha miezi minne, kati ya Octoba hadi January zaidi ya watu 300 waliuawa kwa kupigwa mapanga na silaha nyingine.
Serikali ya Kongo inawatwika jukumu la mauaji hayo wanamgambo wa kiislamu wa ADF - Nalu kutoka nchi jirani ya Uganda - lakini hakuna ushahidi mkubwa kuweza kuthibitisha dhana hizo.
Kwa kuwa sababu za mashambulio hayo ya kigaidi hazijulikani, ndio maana Bahondira anaogopa kurejea nyumbani. "Sikuamini mie kama watu nisiowajua wangenipokea mie na watoto wangu, kwa moyo mkunjufu hivi," amesema bibi huyo mwenye umri wa miaka 30. "Nimeshangaa na zaidi kuliko yote nnafurahi."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/epd
Mhariri: Iddi Ssessanga

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni