Jumanne, 30 Juni 2015

MZIMU WA PESA YA MBOGA WAMKOSESHA USINGIZI MBUNGE, SASA AVAMIA VYOMBO VYA HABARI NA HALIMA MDEE



Prof. Anna tibaijuka akiwa mbele ya jopo la wajumbe wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma wakati akihojiwa hivi karibuni kuhusiana na mgano wa fedha za Akaunti ya escrow.
 
Muleba. Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka amemshambulia Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kwamba vinatumiwa na wabaya wake kumkashifu katika utendaji wake.

Profesa Tibaijuka alitoa shutuma hizo wakati akihutubia wananchi wa Kata ya Bureza. Alisema alikumbwa na kashfa ya Escrow, kutokana na kupata fedha kutoka kwa kaka yake Rugemalila (James) alizompa kusaidia shule anayoisimamia.


Alikanusha tuhuma zilizotolewa na Mdee bungeni dhidi yake kwamba alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kabla ya kuvuliwa wadhifa huo, alikuwa mporaji wa mali za wananchi hasa kumiliki ardhi kubwa.


Alidai kuwa katika kashfa hiyo, kitendo cha kusema fedha aliyoipata ni ya mboga kwa maana ni ndogo imetafsiriwa na kutumiwa na vyombo vya habari, hasa magazeti kumchafua zaidi ndani na nje ya Tanzania.


“Nasema hapa mbele yenu na waandishi wa habari wapo hapa, magazeti yanafanya biashara kupitia kwangu kwani wanapoandika habari zangu magazeti yananunulika kwa haraka siku husika,” alisema Profesa Tibaijuka.


Alilitaja Mwananchi na magazeti mengine pamoja na baadhi yaliyaitwa kuwa ni ya uchwara ambayo alidai kuwa yamenunuliwa na wabaya wake.


Alidai kuwa Mdee alidanganya bungeni kuwa Profesa Tibaijuka ni mporaji ardhi za wananchi kuanzia jimboni na kama isingekuwa ni kinga ya mbunge kutoshtakiwa, angemfungulia mashtaka mahakamani.


Alisema waandishi wa habari wa magazeti hawaandiki mambo mema aliyofanya jimboni badala yake wamesimama kwenye kashfa ya Escrow lakini yeye hafanyi maendeleo yake kwa fedha hizo, bali ana pensheni ya Umoja wa Mataifa (UN).


“Fedha nilizopata Umoja wa Mataifa bado ninazo na Halima Mdee tutakuja kukutana mbele ya safari kama ni pesa ya kula bado ninayo na ile ya Escrow ya Rugemalila ni kuhemea mboga acheni kudanganyika,” alisema Profesa Tibaijuka.


Aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumuunga mkono kwani licha ya kudaiwa kuwa ana umri mkubwa hivyo awaachie vijana, bado yumo na atagombea tena kuwaongoza wananchi akiwa mbunge.


Mdee ajibu mapigo
Akijibu shutuma dhidi yake Mdee alisema alichokisema ni cha kweli na kwamba anao ushahidi kuthibitisha madai yake hayo.“Asiweweseke kwa kuwa hilo suala la uporaji wa ardhi ni la kweli na wala sikumuonea.”MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni