Jumatano, 1 Julai 2015

BASI LAGONGA TRENI LAUA WATANO MOROGORO

Watu wanne wamefariki dunia na 21 kujeruhiwa baada ya basi aina ya Isuzu kugonga treni ya abiria iendayo bara katika kilomita 276/0 kati ya Stesheni za Kimamba na Kilosa mkoani Morogoro saa 11:25 asubuhi leo Julai 01, 2015. Wahanga walipakiwa katika treni hiyo na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Basi lilohusika ni lenye namba za usajili T837CTM Isuzu Coaster linalomilikiwa na Feisal A. Khuwel wa Kilosa.Taarifa kutoka eneo la tukio limefafanua kuwa waliofariki ni wanaume wawili, mwanamke mmoja na mtoto wa miaka minne. Katika majeruhi 21 wako wanaume 14 na Wanawake 7 ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa! Treni ya abiria imeondoka katika Stesheni ya Kilosa saa 3 asubuhi kuendelea na safari yake kwenda Bara. Uongozi wa TRL unawapa pole Ndugu wa Marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta bila ya kutarajiwa na pia inawaombea Marehemu kwa Mola awape mapumziko ya Amani peponi Amina! Hali kadhalika inawaombea majeruhi wapate afueni ya haraka ili warejea katika shughuli zao za kawaida kwa familia zao na Taifa letu.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Elias Mshana Dar es Salaam! Julai 01, 2015



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni