Jumanne, 24 Novemba 2015

MASHARTI YA KUSAFIRI NJE HAYA HAPA

Ofisi ya Rais imesambaza mwongozo unaoweka masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi watatakiwa kutimiza ili wapewe kibali, ikiwa ni mkakati wa kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kudhibiti safari holela za nje.
Rais alitoa agizo hilo baada ya kikao baina yake na makatibu wa wizara kilichofanyika Ikulu siku chache baada ya kuapishwa, akisema ofisi yake ndiyo itakayotoa kibali kwa watumishi ambao wana safari za nje.
Kwa mujibu wa waraka huo, sharti la kwanza linalotakiwa kuzingatiwa na watumishi hao ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Pili, kwa mujibu wa mwongozo huo, maombi yawasilishwe kwa msajili wa hazina kabla ya kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wake na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Tatu, mtendaji mkuu wa shirika au taasisi apime maombi ya safari husika ili kuona kama yana tija na yana umuhimu wa kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kongozi, kabla ya kuwasilishwa kwa msajili wa hazina, kwa mujibu wa mwongozo huo.
Sharti la nne, lina vipengele vitano ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuwasilisha hoja ya safari.
Kipengele cha kwanza ni chanzo cha safari husika, cha pili ni faida yake, tatu kwa nini ni muhimu kwa safari hiyo kufanyika na isipofanyika itaathiri vipi.
Kipengele cha nne kinachambua gharama za safari, kikiweka masharti yanayomtaka mwombaji aainishe gharama ya tiketi ya ndege, posho za safari husika, mlipaji wa gharama za safari na uwezo wa taasisi kifedha.
Kipengele cha tano cha sharti la nne kinamtaka mwombaji aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na Taifa na kama imewahi kufanyika huko nyuma.
Akizungumzia hilo, Balozi Sefue alisema ni kweli ofisi ya Rais ilituma taarifa ya kupiga marufuku safari za nje na kinachofanywa na ofisi za umma ni taratibu za safari hizo zisizoepukika.
Alisema tangu Rais Magufuli apige marufuku safari za nje, ofisi hiyo imesambaza agizo hilo katika ofisi za umma kuwa ni marufuku mtumishi wa umma kusafiri isipokuwa kwa kibali, kiwe cha Rais au cha Katibu Mkuu Kiongozi.
Alisema miongozo ya safari hizo inazitaka ofisi za umma kuhakikisha kuwa ombi la kila anayetaka kusafiri, lichujwe na kuhakikisha safari yake haiepukiki.
“Ofisi inapoleta maombi kwetu ijiridhishe kuwa haiepukiki. Maombi mengi yataishia kwenye ofisi zao, ikija kwetu inatakiwa ionyeshe wazi kuwa haiepukiki na tukipima vigezo vyake na kuona haviridhishi, tunaweza kuikataa vile vile,” alisema.
Alisema miongozo iliyobandikwa katika ofisi za umma kuhusu safari za nje ni taratibu ambazo zinafuatwa na taasisi baada ya agizo hilo kutoka ofisi ya Rais.
Ofisi za umma zilipokea barua kutoka kwa msajili wa hazina, yenye kumbukumbu namba CEA.111/372/01 iliyowasilishwa Novemba 12 mwaka huu ikielekeza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla la safari za nje ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake.
Zuio hilo linayagusa mashirika na taasisi zote za umma. Barua hiyo ya msajili ilieleza kuwa zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.
UDSM wapokea agizo
Habari za kuwapo kwa agizo hilo zilithibipitishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, ambaye alikiri kupokea maelekezo kutoka kwa msajili wa hazina.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni