Jumatatu, 8 Februari 2016

WATU 2 WATOLEWA WAKIWA HAI TAIWAN

 Mwili
  Mwili wa mumewe mwanamke huyo huenda ulimkinga
Watu wawili wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka kufuatia tetemeko la ardhi mjini Tainan, Taiwan.
Wa kwanza alikuwa mwanamke ambaye maafisa wanasema alipatikana chini ya mwili wa mumewe. Mwili wa mtoto wao wa umri wa miaka miwili ulipatikana karibu nao.
Muda mfupi baadaye, mwanamume mmoja pia alipatikana akiwa hai, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Watu 37 walifariki baada ya tetemeko la ardhi la nguvu ya 6.4 kwenye vipimo vya Richter kukumba taifa hilo.
Wengi wa waliofariki walikuwa katika jumba la Weiguan Jinlong, ambapo zaidi ya watu 100 bado wanaaminika kukwama kwenye vifusi.
Mwanamke aliyeokolewa, Tsao Wei-ling, aliokolewa Jumatatu asubuhi, mbunge wa eneo hilo Wang Ting-yu alinukuliwa akisema na shirika la habari la Reuters.
Alikuwa bado hajapoteza fahamu na alikimbizwa hospitalini.
Waokoaji wanasema ni kana kwamba mwili wa mumewe ulimkinga dhidi ya nguzo iliyowaangukia.
Taiwan
Watu 310 wameokolewa kufikia sasa
Jamaa watano wa familia hiyo bado hawajulikani waliko.
Mwanamume huyo mwingine aliyeokolewa alikuwa akizungumza na waokoaji usiku wote kabla ya kuokolewa mchana.
Msichana wa umri wa miezi sita aliyeokolewa akiwa hai awali alifariki baadaye akitibiwa hospitalini.
Jumba la Weiguan Jinlong (Dragoni wa Dhahabu) lilikuwa na ghorofa 17. Uchunguzi unafanywa kubaini iwapo udhaifu katika ujenzi wake ulichangia kubomoka kwake

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni