Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, alisema jana kuwa Sarah
alifariki dunia juzi saa moja jioni, katika Hospitali ya Wilaya ya
Njombe ya Kibena, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.
Alisema mkuu huyo wa wilaya aliugua ghafla juzi muda mfupi baada ya
kutoka ofisini na alianza kujisikia vibaya alipokuwa akijiandaa kula
chakula alichokuwa ameandaliwa.
“Mkuu wa wilaya alipofika nyumbani kwake, alitaka kupata chakula
lakini alianza kupata shida ya kupumua na baadaye kuanza kulegea mwili.
Alipelekwa katika Hospitali ya Kibena ndipo umauti ukamfika akipatiwa
matibabu,” alisema Dk. Nchimbi
Dk. Nchimbi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali
Teule ya Wilaya ya Wanging’ombe ya Ilembula, ambayo ndiyo ina uwezo wa
kuhifadhi maiti.
Alisema mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na kwamba leo
kutakuwa na ibada maalum ya kuaga mwili wake katika Kanisa Kuu la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini mjini hapa,
alikokuwa akiabudu.
Mkuu wa Mkoa alisema baada ya hapo, mwili wa marehemu utasafirishwa
kwenda Dar es Salaam, ambako familia yake inaishi maeneo ya Kigamboni,
kwa maziko ambayo yatafanyika siku ya Alhamisi tarehe 24/3/2016.
Sarah alianza kazi ya ukuu wa wilaya mwaka 2006 katika wilaya ya
Kilindi mkoani Tangana baadaye kuhamia Njombe (wakati huo ikiwa katika
mkoa wa Iringa) na sasa mkoa wa Njombe, alikotumika hadi kufariki dunia.
Kabla ya kuwa mkuu wa wilaya, alikuwa mwandishi wa habari na
mtangazaji wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) sasa Shirika
la Utangazaji Tanzania (TBC).
MAGUFULI ATUMA SALAMU
Katika hatua nyingine, Rais Dk. John Magufuli amemtumia salamu za
rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, kutokana na kifo
cha ghafla cha mkuu huyo wa wilaya.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli alielezea kushtushwa na kifo cha
ghafla cha Sarah Dumba, ambaye alisema alimfahamu kwa uchapakazi wake,
uaminifu na uadilifu katika utumishi wa umma na uongozi.
"Nimeshtushwa sana na kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah
Dumba. Kwa mara nyingine, taifa limempoteza mtu muhimu ambaye mchango
wake ulikuwa bado unahitajika," alisema kama alivyonukuliwa katika
taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu,
Gerson Msigwa.
Dk. Magufuli alibainisha kuwa Sarah Dumba atakumbukwa kwa kazi
kubwa aliyoifanya ya kuhimiza maendeleo ya wananchi, hususan katika
kilimo na ufugaji, nidhamu ya utumishi serikalini na kuwatetea wananchi
wa hali ya chini, wakati wotealipokuwa mkuu wa wilaya.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli alisema anaungana na familia ya
marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo, katika
kipindi hiki kigumu na pia amewataka wote kuwa na subira na uvumilivu.
TAMWA YAMLILIA
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema kimepokea
kwa masikitiko taarifa ya kifo cha mwanachama wake ambaye alikuwa
mwanahabari mahiri na mkongwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga, alisema chama hicho
kinaungana na familia ya marehemu, serikali, wanahabari na Watanzania
wote katika kuombeleza kifo hicho na kwamba ameacha pengo kubwa kwenye
tasnia ya habari, hasa wanawake na taifa kwa ujumla.
Sarah Dumba amewahi kuwa mtangazaji wa RTD na wakati fulani
aliteuliwa kuwa mwakilishi wa chombo hicho mkoa wa Morogoro kuanzia
mwaka 1998 hadi 2006 alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya.
Kitaaluma, Sarah Dumba alisomea mafunzo ya utangazaji Cairo, Misri
na baadaye alijiunga na Chuo cha Diplomasia, Kurasini jijini Dar es
Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni