Jumatatu, 14 Machi 2016

JPM ATEUA WAKUU WA MIKOA

Baada ya uteuzi wa mawaziri na makatibu wakuu, Rais John Magufuli, ameteua wakuu wa mikoa 26, kati yao 10 ni wapya wakiwamo Mameja Jenerali na Brigedia Jenerali 16 waliostaafu jeshi Machi 4, mwaka huu na wabunge wanne walioshindwa kutetea nafasi zao.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, inaonyesha kuwa waliokuwa wakuu wa wilaya watatu chini ya Serikali ya Jakaya Kikwete, wamepandishwa na kuwa wakuu wa mikoa, sita wamehamishwa vituo vya kazi na saba wamebaki vituo vya awali.
Kutokana na idadi hiyo, wakuu wa mikoa ambao walikuwa chini ya Serikali ya Kikwete waliobaki ni 16.
Pia, Rais Magufuli amemthibitisha Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, kushika rasmi nafasi hiyo na Valentino Mlowola, kuwa  Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), awali walikuwa wakikaimu nafasi hizo.
wanajeshi washaafu waula
Wanajeshi wastaafu walioteuliwa ni Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Elias Kyunga, aliyekuwa Chuo cha Kamanda na Unadhimu (JWTZ) ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu, aliyekuwa Mkuu wa Kamandi ya Nchi Kavu anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) sasa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, aliyekuwa Makao Makuu ya Jeshi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Wakuu wa wilaya waliopanda 
Aidha, katika uteuzi huo wakuu wa mikoa wapya walioteuliwa ni Paul Makonda aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Antony Mtaka (Simiyu) huku Kamishna Mstaafu wa Polisi Zerote Steven, aliyekuwa Mkuu Wilaya ya Musoma (Rukwa).
Wabunge waliomwagwa waula
Wakuu wa mikoa wapya waliokuwa wanasiasa, ni aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbozi, Godfrey Zambi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Anna Kilango aliyekuwa Mbunge Same Mashariki(Shinyanga), aliyekuwa Mbunge wa Serengeti na Naibu Waziri wa Afya wa serikali ya awamu ya nne, Steven Kebwe (Morogoro).
Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Siha, Aggrey Mwanri amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, aliyekuwa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Methew Mtigumwe (Singida) na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Martine Shigela (Tanga).
 
WALIOHAMISHWA
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Magufuli amewahamisha wakuu wa mikoa ambao ni Jordan Rugimbana aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi na kuhamishiwa Dodoma, Said Meck Sadick aliyekuwa jijini Dar es Salaam amehamishiwa Kilimanjaro na Magesa Mulongo, aliyekuwa Mkoa wa Mwanza sasa amehamishiwa Mara.
Wengine ni Amos Makalla, aliyekuwa Mkoa wa Kilimanjaro, amehamishiwa Mbeya, John Mongella na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na  amehamishiwa Mwanza.
 
WALIOBAKISHWA
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Wakuu wa mikoa ambao Rais Magufuli, amewabakisha kwenye mikoa waliyokuwapo awali ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Juma Masenza, Rehema Nchimbi (Njombe), Mhandisi Evarist Ndikilo,  (Pwani) na Said Thabit Mwambungu (Ruvuma).
Pia Rais Magufuli, amemteua Luteni Mstaafu Chiku Galawa kuwa Mkuu wa Mkoa mpya wa Songwe, awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
WALIOTEMWA
Katika uteuzi huo, pia kuna wakuu wa mikoa ambao hawajateuliwa na Rais Magufuli kuendelea kushika nafasi hiyo, ambao ni Erasto Mbwilo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Kone, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu, Issa Machibya na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajab Rutengwe.
Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwasa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Ibrahim Msengi.
Wakuu wa mikoa wengine walioachwa ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Said Magalula na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Anseri Msangi.
Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa, wataapishwa kesho Machi 15 saa 3:30 Ikulu, Jijini Dar es salaam.
WACHAMBUZI WAZUNGUMZA
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk. Wetengere Kitojo, alisema Rais Dk. Magufuli amefanya uteuzi huo wa wakuu wa mikoa kimpango zaidi.
Alisema uteuzi wa askari wastaafu kuongoza mikoa ya pembezoni mwa nchi ni kuhakikisha wanaimarisha usalama wa nchi.
Alisema mikoa hiyo ni ya kimkakati na ni maeneo ambayo vitendo vya kihalifu na kigaidi ni rahisi kutokea, hivyo rais amefanya uteuzi huo ili kudhibiti na kujihami na hali hiyo.
Alisema kuachwa kwa baadhi yao na wengine kuendelea nao, kunatokana na uzoefu na kwamba huenda ni mkakati wa kuimarisha utendaji wa kazi serikalini.
Alisema uteuzi wa Makonda ulitegemewa na wananchi wengi kwa kuwa kwa kipindi kifupi alichoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ameonyesha uchapakazi wa hali ya juu.
Naye Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Iringa (IuCo), Ordination Mgongolwa, alisema uteuzi wa majenerali wastaafu kuongoza mikoa ya Geita, Kagera, Katavi na Rukwa ni kuhakikisha nchi inakuwa na usalama wa kutosha.
Alisema wanajeshi hao wana ujuzi mkubwa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi unakuwapo na kwamba ni uteuzi uliozingatia tija.
Alisema Rais Magufuli ameendelea na baadhi ya wakuu wa zamani wa mikoa, ameona utendaji wao wa kazi ni mzuri na wanaweza kwenda sawa na kaulimbiu ya ‘Hapa kazi tu’.
“Ila kuna baadhi ya wakuu wa mikoa sijawakubali, siwezi kuwataja, lakini katika utawala wa Rais Kikwete walikuwapo na sasa wamerudishwa, hawakufanya maendeleo yoyote, pengine wanaweza kubadilika na kuendana na kasi ya Magufuli,” alisema Mgongolwa.
Kuhusu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mulongo, ambaye katika mabadiliko hayo amehamishiwa Mkoa wa Mara, alisema ni uteuzi wa kawaida na uliotegemewa kwa kuwa Mulongo alionyesha tangu awali kukipigania Chama Cha Mapinduzi (CCM) pindi alipokuwa akishikilia nafasi hiyo katika mikoa ya  Arusha na Mwanza.
Mhadhiri katika Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Siasa ya Sayansi, Bashiru Ally, alisema tangu nchi ipate uhuru wakuu wa wilaya na mikoa walikuwa ni watu wenye umuhimu mkubwa.
Alisema haikuwa rahisi kwa askari aliyestaafu jeshi kumruhusu kwenda uraiani, na kwamba walikuwa wanapewa vyeo mbalimbali serikalini vikiwamo vya ukuu wa mikoa na wilaya.
“Miaka ya nyuma nafasi ya ukuu wa wilaya au mikoa ilikuwa ni sehemu ya kulipa fadhila, kwa mfano meja jenerali ametoka kwenye vita na amestaafu, hivyo anapelekwa kuwa mkuu wa mkoa, wilaya au balozi,” alisema Bashiru.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni