Uamuzi huo umetangazwa na Idara ya Ofisi ya Hazina inayoshughulikia udhibiti wa mali za nje ya Marekani (OFAC).
Marekani imepeleka suala hilo katika Bunge la Congress.
Aidha, Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (International Narcotic Control Board-ICBC), juzi ilitoa ripoti ya mwaka 2015 iliyolenga Afrika na Tanzania, ikionyesha kuwa Tanzania ni kichochoro cha kupitisha dawa za kulevya.
Taarifa ya Marekani iliyochapishwa kwenye Mtandao wa OFAC, ilimhusisha Mtanzania huyo na Kampuni yake ya Hassan Drug Trafficking Organization, kama mfanyabiashara muhimu wa kigeni wa mihadarati kwa mujibu wa Sheria ya Wafanyabiashara wa Kigeni wa Mihadarati (The Foreign Narcotics Kingpin Designation Act), Kingpin Act ya nchi hiyo.
“Hassan ni mfanyabiashara mkubwa wa kimataifa wa mihadarati anayesafirisha kwa siri tani za shehena za mihadarati aina ya heroin na cocaine kwenda Afrika, Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini, kupitia kampuni yake hiyo yenye makao Afrika Mashariki.
“Kwa mujibu wa uamuzi huu wa leo (Machi 9), mali zake zote na za kampuni yake ambazo zipo kwenye mamlaka ya Marekani ama ambazo zipo katika udhibiti wa watu wa Marekani, zinataifishwa na watu hao kwa ujumla wanakatazwa kujihusisha na mali hizo,” inaeleza taarifa hiyo.
Inaeleza kuwa, baada ya kuwindwa kwa muda wa miaka miwili mfululizo, Hassan alikamatwa mwaka 2014, na mamlaka za Tanzania akihusishwa na kusafirisha kilo 210 za heroin, zilizokamatwa Januari 2012 mkoani Lindi.
Inasema Hassan amejaribu mara kwa mara kuwahonga maofisa wa Serikali za Kiafrika ili kukwepa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka, kutokana na shughuli zake hizo za biashara ya mihadarati.
“Hatua ya leo inaweka vikwazo kwa Ali Khatib Haji Hassan na mtandao wake haramu wa biashara ya mihadarati, kwa kusafirisha kwa magendo heroin na cocaine duniani, akilenga kutumia faida haramu kuwahonga maofisa wa Serikali za Kiafrika,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa OFAC, John E. Smith.
“Wafanyabishara wa mihadarati kama ilivyo kwa Kampuni ya Hassan, wanasababisha tishio kubwa kwa mfumo wa fedha wa kimataifa na utulivu wa kikanda, na idara inabaki imara kuwaibua na kuwalenga wale wote wanaochochea biashara ya mihadarati duniani,” ilieleza.
Inasema Kampuni ya Mihadarati ya Hassan, inapata kiwango kikubwa cha heroin kutoka kwa vyanzo vilivyoko Kusini Magharibi mwa Asia, pamoja na kiwango kikubwa cha cocaine kutoka kwa wasambazaji walioko Marekani ya Kusini.
“Tangu mwaka 2006, Hassan amewaelekeza wanachama wa mtandao wake, kupeleka shehena ya heroin katika maeneo yaliyopo China, Ulaya na Marekani.
“Hassan alitumika kama msambazaji wa msingi kwa wafanyabiashara wa mihadarati walio na makao Tanzania, akipokea mara kwa mara mamia ya kilo za heroin, zilizosafirishwa kwa njia ya bahari kutoka pwani ya Makran nchini Pakistan na Iran.
“Hassan, pia alisimamia mtandao mkubwa wa mihadarati Amerika ya Kati uliosambaza cocaine ya Amerika ya Kusini na Afrika Mashariki ikiwa njiani kwenda Ulaya na China,” inaeleza taarifa hiyo.
Inaeleza kuwa, Juni 2000, zaidi ya vyombo na watu binafsi 1,800 vimetajwa kwa mujibu wa sheria hiyo ya Marekani kushiriki kwenye biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya.
Idara hiyo, pia imemwandikia mwenyekiti wa Bunge la Congress, wenyeviti wa Kamati za Usalama, Mambo ya Nje, Kamati ya Seneti ya Huduma ya Vyombo vya Ulinzi na Mahakama na ile ya uhusiano wa kimataifa na fedha kuhusu suala hilo.
Ripoti ya Mtanzania huyo imepelekwa kwa mihimili hiyo kama ambavyo sheria za nchi hiyo zinataka watu wa kigeni wanaostahili kuwekewa vikwazo chini ya sheria hiyo (Kingpin Act) na vikwazo, kutokana na kosa lake.
Mkuu wa Polisi wa Kimataifa Interpol, Gustavus Balile, akizungumza na Nipashe jana alisema, Hassan baada ya tukio la nchini Mmarekani, alihusishwa pia na lile la dawa za kulevya kilo 201 zilizokamatwa mkoani Lindi na kwamba kwa sasa yuko gerezani.
Watu waliokamata na dawa hizo za Lindi aina ya Heroin zenye thamani iliyokadiriwa kuwa ya Sh. bilioni 9.4, ni pamoja na Maureen Liyumba.
Balile alisema Hassan alikamatwa mwaka mmoja baada ya tukio hilo la Lindi na kwamba kesi yake bado inaendelea mahakamani.
Alipoulizwa kama kuna uvunjifu wa sheria yoyote kuhusu majadiliano ya mtu huyo yanayoendelea katika Bunge la Marekani, Balile alisema kwa sababu Marekani inasheria zake, wanaruhusiwa kufanya hivyo.
“Wao wanamjadili kulingana na sheria zao, na makosa waliyomkuta nayo huko, hivyo hawawezi kuzuiwa kujadili wala hawaingilii uhuru wa mahakama yetu,” alisema.
Kuhusu kutaifisha mali zake anazomiliki Tanzania kama walivyofanya Marekani, Balile alisema itategemea uamuzi wa mahakama endapo patakuwa na maombi ya kufanya hivyo.
Ripoti ya Kimataifa yanyooshea Tanzania kidole
Ripoti ya Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Afrika na Tanzania kwa mwaka 2015, iliyotolewa Machi 9, mwaka huu na ICBC, inasema kwa mwaka 2014, Tanzania ilitumika zaidi kupitisha dawa za kulevya.
Ripoti hiyo inasema kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kilichokamatwa kilikuwa ni Bangi, Mirungi na Heroin.
“Katika miezi minane ya mwaka 2014, vyombo vya dola vilikamata zaidi ya kilo 321 za heroin, kiasi ambacho ni zaidi ya kilichokamatwa mwaka 2013.
“Heroin iliyokamatwa ilikuwa ikisafirishwa kutoka Afghanistan, India, Iran na Pakistan na ilikuwa ikipelekwa China, Japan, Afrika Kusini, Uturuki, Amerika na nchi za Bara Ulaya.
"Aidha, tani tatu za cocaine zilikamatwa zikiwa ndani ya meli iliyosajiliwa Tanzania Aprili 205. Meli hiyo ilizuiwa na mamlaka za Uingereza ikiwa maili 100 kusini mwa pwani ya Scotland,” inaeleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Bara la Afrika liliendelea kutumika kupitisha dawa za kulevya. Afrika Magharibi ilitumika mara kwa mara kupitisha Cocaine na dawa nyingine kuelekea Bara la Ulaya wakati Afrika ya Kaskazini iliendelea kuwa chanzo kikuu cha dawa zilizoingia barani Ulaya.
Inaeleza kutumika kwa Afrika ya Mashariki kama kitovu cha kusafirisha heroin iliyotokea Afghanistan ikipelekwa Bara la Ulaya kuliongezeka. Hali hii inachukuliwa kuwa ndiyo sababu ya kuongezeka kwa matumizi ya heroin katika eneo la Afrika ya Mashariki.
Usafirishaji wa heroin kutoka Afghanistan kupitia Afrika Mashariki ulionekana kushika kasi mwaka 2014. Hali hii inaashiriwa na kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha dawa za heroin katika nchi za Kenya na Tanzania.
Inaeleza kuwa kilo 387 za heroin zilikamtwa kwa mkupuo mmoja katika Bandari ya Mombasa, lita 3,200 za maji yaliyochanganywa na heroin na lita 2,400 za mafuta ya dizeli yaliyochanganywa na heroin zilikamwatwa nchini Kenya mwaka 2014.
Kadhalika, inaeleza kilo 321 za heroin zilikamatwa nchini Tanzania mwaka 2014.
“Imeripotiwa kuwa usafirishaji wa dawa za kulevya hufanywa kwa kutumia meli kubwa ambazo hutia nanga katika bahari kuu na kushusha mizigo yenye dawa hizi kwenye majahazi, mashua, boti ziendazo kasi au hata ngalawa ambazo husafirisha mizigo hiyo hadi nchi kavu.
“Dawa hizi zimekuwa zikipitia Afrika Mashariki zikipelekwa Italia, Uholanzi, Uingereza na Amerika. Nchi nyingine barani Afrika ambazo zimeripoti kuwapo kwa ukamataji wa heroin ni Misri, Algeria na Morocco,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inaeleza Bara la Afrika kuna watumiaji wa bangi wengi na kwamba kati ya watu 100 wenye umri wa miaka kati ya 15 na 64, nane wanatumia dawa hizo za kulevya.
Inaeleza heroin ni dawa ya pili kwa kutumika zaidi barani Afrika na kwamba inakadiriwa kuwa watu watatu kati ya 1,000 wenye umri kati ya miaka 15 na 64 hutumia dawa hizo. Cocaine ni dawa ya tatu kwa kutumiwa zaidi barani Afrika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni