Jumatano, 16 Machi 2016

MWIGULU NCHEMBA AANZA SAFARI YA KUHAKIKISHA WAFUGAJI WANAACHA KUFUGA KIHOLELA,WAFUGE KWA VITALU.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mh:Mwigulu Nchemba akimuangalia  dume la ng’ombe linalotumika kuzalisha Mitamba kwenye kitalu namba 9 shamba la Kitengule-Karagwe.
Baadhi ya ng’ombe waliopo kitalu namba 9 shamba la Kitengule ambapo kwenye block hii moja kuna ng’ombe zaidi ya 800 wanaolishwa na kuhudumiwa vizuri na mmiliki wa kitalu hiki
.Ng’ombe wakitoka kuogeshwa kwa ajili ya kuua baadhi ya wadudu kama kupe wanaopendelea kukaa kwenye mwili wa ng’ombe. Hili ni moja ya josho la kisasa ndani ya kitalu namba 9.

Kufuatia ziara ya Waziri mkuu,Mh:Kassim Majaliwa ndani ya mkoa wa Kagera akiwa ameambatana na waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani, Ziara hiyo imekuja na maagizo kadhaa ikiwamo wamiliki wote wa vitalu kwenye ranchi za Taifa ambao hawajaviendeleza waviachie mara moja na maeneo hayo yagawiwe upya, Waziri Mkuu ameagiza pia kwa wamiliki wa vitalu ambao sio watanzania wajisalimishe au waondoke kwenye vitalu hivyo kabla hatua kali hazijaanza kuchukuliwa.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mh:Mwigulu Nchemba akiwa na timu yake ya wataalamu wameshaanza kupitia vitalu vyote na wamiliki wake ikiwepo pia idadi ya mifugo kwa kila kitalu. Mwigulu Nchemba amekutana na wamiliki wa vitalu kwenye shamba la Kitangile-Karagwe na kuagiza vitalu vyote ambavyo havijaendeleza kuchukuliwa na serikali kwa ajili ya kuwapatia watanzania wenye uwezo wa kuviendeleza.

Mwigulu Nchemba ameagiza pia wamiliki wa vitalu kuacha mchezo wa kukodisha na kuingiza mifugo kutoka kwa wafugaji wa nchi jirani, kitendo hicho ni kosa na yeyote atakayebainika atakabiliwa na adhabu kali. Mbali na vitalu hivyo, Waziri Mkuu akishirikiana na Waziri wa Kilimo wameagiza ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera kuondoa wavamizi wote kwenye mapori tengefu ya serikali kabla hatua zingine kuanza kutekelezwa.
Kupitia uwekezaji mzuri kwenye kitalu namba 9 cha shamba la Kitengule, Mwigulu Nchemba ametoa rai kwa wafugaji wote nchini kuanza kujipanga kufuga kwa mfumo wa vitalu ili kuachana na ufugaji holela unaopelekea migogoro mbalimbali na wakulima.
Picha/Maelezo na Festo Sanga Jr.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni