SEPTEMBA 10, mwaka huu, saa 9 na dakika 27 mchana kulitokea tetemeko
la ardhi mkoani Kagera. Kitovu cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya
latitudo 10 06’ na longitudo 31055’, eneo ambalo ni kilomita 20,
Kaskazini Mashariki mwa Kijiji cha Nsunga na kilomita 42 Kaskazini
Magharibi mwa mji wa Bukoba. Kitovu hicho kilikuwa kilomita 10 chini ya
ardhi kwenye eneo hilo.
Nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli
ya “Richter”, ukubwa ambao ni wa juu sana, kiasi cha kuleta madhara
makubwa.
Kutokana na ukubwa huo, maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera ikijumuisha
mji wa Bukoba, yamepatwa na madhara makubwa ikijumuisha nyumba nyingi
kupasuka, watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za
nyuma, ambapo pia watu 16 wamepoteza maisha yao.
Sababu za kutokea tetemeko hilo
Kwa kuwa kitovu cha tetemeko hilo kiko chini sana ya ardhi (Kilometa
10) na kwa kutafsiri umbile la mawimbi ya tetemeko hilo yaliyonakiliwa
na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi, inaonekana kuwa tetemeko hilo
lilitokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na
mipasuko ya ardhi, mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa.
Kwa kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi, liko karibu na
mkondo wa Magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki, inakisiwa kuwa
mtetemo huo umesababishwa na kuteleza na kusuguana kwa mapande ya miamba
juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Upimaji wa matetemeko ya ardhi
Mpaka sasa hapa nchini na duniani kote, hakuna vifaa au taratibu za
kuweza kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi. Vifaa vyote na taratibu
zote za kuratibu/kupima matetemeko ya ardhi, vinapima ukubwa na tabia
ya tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
Tafiti za kina
Wakala wa Jiolojia Tanzania umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo.
Taarifa zaidi juu ya tukio hilo, zitaendelea kutolewa kulingana na
matokeo ya tafiti hizo pamoja na tafsiri ya taarifa na takwimu za
matetemeko ya ardhi, zinazonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya
ardhi nchini, hususani Kituo cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu na
eneo la tetemeko hilo.
Mambo muhimu ya kuzingatia kuepuka madhara ya tetemeko la ardhi
(i) Kabla ya tukio Kwanza elimu ya tahadhari inapaswa itolewe ili
kila mmoja aelewe nini cha kufanya, linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa
ni pamoja na kupata mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu
namna ya kuhudumia majeruhi ama waathirika; na pia jeshi la zimamoto ili
kupata elimu kuhusu namna ya kutumia kizimamoto.
Elimu na mafunzo hayo, yatasaidia kuwaweka watu katika hali ya
tahadhari; na hii itasaidia kupunguza taharuki wakati wa tukio, kwa vile
watakuwa sasa wanajua namna ya kuchukua tahadhari.
Pili; kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari hizo mara kwa mara ili
kujizoesha, kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo,
watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwani huwa bado
wanajiuliza kwamba wafanye nini. Hivyo mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi
ya kuchukua tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio
linapotokea.
Tatu; wananchi pia wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa
kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa
ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa
kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo, kuepuka
ujenzi wa nyumba katika miinuko mikali yenye kuambatana na mawe/ miamba
na kuepuka ujenzi wa makazi katika maeneo tete yenye mipasuko ya miamba
(faults) na uwezekano mkubwa wa kutokea matetemeko.
(ii) Wakati wa tukio Kwanza wakati wa tukio la tetemeko la ardhi,
unashauriwa kukaa mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na
majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali ya ardhi. Watu
wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika sehemu za uwazi.
Pili; endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba, unashauriwa
ukae chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta
na pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha
ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.
Tatu; unashauriwa usitembee umbali mrefu kwa lengo la kutafuta mahali
salama kwa sababu tetemeko la ardhi, hutokea ghafla na huchukua muda
mfupi. Takwimu zinaonesha kwamba watu wanaotaharuki na kukimbia ovyo
wakati wa tukio la tetemeko ndio hupata madhara ama kuumia.
Nne; salimisha macho yako kwa kuinamisha kichwa chako wakati wa tukio.
Tano; baki mahali salama hadi hapo mitetemo itakapomalizika na kisha
ujikague kuona kama hujaumia na ndipo utoe msaada kwa wengine ambao
watakuwa wameumia. Sita; ondoka mahali ulipo kwa uangalifu, kuepuka vitu
ambavyo vitakuwa vimedondoka na kuvunjika kwani vinaweza kukudhuru.
Saba; jiandae kwa mitetemo itakayofuata baada ya mtetemo mkuu.
Tetemeko kuu huwa mara nyingi linafuatiwa na mitetemo mingi midogo
midogo. Nane; kumbuka kuwa matukio ya matetemeko ya ardhi, huweza
kuambatana na moto hivyo jihadhari na matukio ya moto, kwa vile tetemeko
la ardhi linaweza kusababisha kupasuka kwa mabomba ya gesi au kukatika
kwa nyaya za umeme ama kuharibika kwa vifaa vinavyotumia umeme na
kusababisha hitilafu ya umeme.
Tisa; kama uko nje ya jengo wakati tetemeko linatokea, unashauriwa
kubaki nje, simama mahali pa wazi na uwe mbali na majengo, miti mikubwa,
nguzo na nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana kwani
paa za nyumba, miti, nguzo na nyaya za umeme vinaweza kudondoka na
kuleta madhara.
Kumi; endapo utakuwa unaendesha chombo cha moto wakati wa tukio la
tetemeko la ardhi, unashauriwa usimame kwa uangalifu sehemu salama na
usubiri hadi mitetemo imalizike, ndipo uendelee na safari yako kwani
tetemeko linaweza kusababisha barabara au madaraja kukatika.
Kumi na moja; endapo utakuwa kwenye maeneo ya miinuko au milima, uwe
mwangalifu ili kuepuka kuporomokewa na mawe au kuangukiwa na miti.
Kumi na mbili; baada ya mitetemo kumalizika, endapo itakulazimu
kuondoka mahali ulipo ukiwa katika jengo refu, unashauriwa kutumia ngazi
badala ya lifti au kipandishi.
iii) Baada ya tukio: Kwanza, wananchi wanashauriwa baada ya tukio,
kuzima umeme katika majengo ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme,
kwani mitetemo huenda ikaendelea tena.
Pili; kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata
madhara kama vile nyufa n.k, na kwamba yanaweza kuendelea kutumika na
kama ikibidi, basi unashauriwa kuwaita wataalamu wa majengo ili
wayafanyie ukaguzi.
Tatu; endapo utaangukiwa na vitu vizito, usijaribu kutumia nguvu
nyingi ili kujinasua kwani hujui vitu hivyo vina uzito kiasi gani, omba
msaada kwa kuita kwa sauti, lakini usifanye hivyo mara nyingi ili
usipoteze nguvu nyingi mwilini maana hujui ni lini utaokolewa.
Nne; toa msaada unaowezekana kwa watu walioathirika na tetemeko na utoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika na uokoaji
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni