Alhamisi, 3 Agosti 2017

Bangi ekari 10 zateketezwa Mpwapwa

KATIKA kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma imeweza kuteketeza ekari 10 za mashamba ya bangi huku watuhumiwa 34 walipatikana na dawa za kulevya aina ya bangi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri, wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya zilizo katika mapambano ya dawa za kulevya, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Juni 2017, wilaya hiyo iliweza kuteketeza mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 10 katika maeneo matatu tofauti.
Pia alisema kwa nyakati tofauti, jumla ya watuhumiwa 34 walikamatwa baada ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi. Alisema kati ya watuhumiwa waliokamatwa, 16 walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo kati ya mwaka moja hadi miaka 30 pamoja na kulipa faini.
Pia alisema bangi iliyokamatwa ni gunia moja, kilo moja na gramu 542, misokoto tisa na kete 121. Shekimweri alisema wilaya inaendelea kutoa elimu kwa vijana wasijiingize katika matumizi ya dawa za kulevya ambapo pia wilaya imeanzisha kikundi cha vijana cha waliokuwa wanatumia dawa hizo ili waweze kuwaelimisha wenzao madhara ya dawa hizo na kuziepuka.
Cha kujiuliza ni kwa nini bangi ikubali kuota kila mahali hata kwenye ukame kama Dodoma?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni