Chuo Kikuu kimoja nchini Afrika Kusini kimesema kwamba kilituma kimakosa jumla ya randi milioni 14 ambazo ni sawa na dola milioni moja za Marekani katika akaunti ya benki ya mwanafunzi mmoja nchini humo.
Pesa hizo zilitoka kwenye mfuko wa shirika la kufadhili wanafunzi kimasomo nchini humo NSFAS.
Chuo Kikuu cha Walter Sisulu, kinasema kuwa pesa hizo ziliwekwa miezi mitano iliyopita, huku makosa hayo yakijulikana baada ya risiti ya akaunti ya mwanafunzi huyo kuonyesha kuwa na mamilioni ya pesa baada ya kuwekwa katika mtandao wa kijamii.
Chuo hicho kikuu sasa kinachunguza ni kwa nini mwanafunzi huyo hakupiga ripoti ya kuwepo kiasi kikubwa hivyo cha pesa kwenye akaunti yake.
Mwanafunzi huyo amekanusha madai hayo.
Ripoti ya shirika la habari la EWN inasema picha zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha mwanafunzi huyo wa kike huyo akijisifu na kujionyesha kwenye sherehe moja huku akijiburudisha na vitu vizuri vizuri, kama vile simu mpya ya rununu.
Inaaminika kwamba mwanafunzi huyo tayari ametumia randi 400,000.
Msemaji wa Chuo hicho Kikuu Yonela Tukwayo, amesema kuwa pesa hizo ziliwekwa kwenye akaunti hiyo kimakosa na kampuni ambayo inasimamia fedha za hazina ya kitaifa za msaada wa karo ya wanafunzi (NSFAS) ambayo inajulikana kama Intellicard na kwamba ni sharti mwanafunzi huyo arejeshe fedha hizo:
''Pia tunaangalia sheria za NSFAS, inayoonyesha mtoto huyo alitia saini makubaliano ya kukubali....Masharti ya matumizi ambayo fedha hizo zinafaa kutumika.
Kwa hivyo itabidi mwanafunzi huyo alipe kila senti ya fedha alizotumia, hata akilipa kwa miaka 20 na zaidi."
Gazeti moja nchini Afrika Kusini limewauliza wasomaji ni kwa njia gani wangetumia pesa nyingi kama hizo iwapo wangeamka na kuzipata kwenye akaunti.
Shirika la habari la News24 baadaye limemnukuu msemaji wa chuo kikuu hicho Yonela Tukwayo, akisema kuwa kuhamishwa kwa fedha hizo hadi kwenye akaunti isiyokusudiwa, yalikuwa ni makosa ambayo yangekunduliwa na NSFAS, ambayo inasimamia malipo hayo.
NSFAS imekanusha madai hayo kupitia msururu wa ujumbe kwenye Twitter, huku ikisema kuwa siyo yenye kulaumiwa kwa makosa hayo.
Bi Tukwayo anasema kuwa, mwanafunzi huyo tayari ametumia, dola 38,000 (£30,000), huku akitakiwa kulipa kila ''senti aliyotumia''.
Ripoti hiyo inasema kuwa mwanafunzi huyo anashikilia wadhifa wa uongozi katika chama cha wanafunzi wa Chuo Kikuu.
Mwenzake katika chama hicho cha wanafunzi wa Chuo Kikuu, ameiambia News24 kuwa, ujumbe katika mtandao wake wa kijamii wa Facebook unadai kuwa amepokea fedha hizo kwa njia halali.
Je wewe ungefanya nini ikiwa ni wewe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni