RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amesema hali ya elimu nchini ni mbaya. Kutokana na hali hiyo, amesema yanahitajika mapinduzi makubwa haraka ili kunusuru tatizo hilo.
Alisema mbali na hali hiyo, anapata shida na uamuzi wa Serikali kubadili madaraja ya ufaulu, hali inayozidi kuliangamiza Taifa.
Mkapa alitoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam jana, wakati wa ibada ya kuaga mwili wa mke wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Utumishi katika Serikali ya Awamu ya Tatu, marehemu Alice Rugumyamheto, aliyefariki dunia Desemba 25, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, iliyofanyika katika Kanisa la St. Alban, Upanga, mjini Dar es Salaam jana, Mkapa alisema hali ya elimu nchini inahitaji mageuzi ya kina kuliko kuacha hivi ilivyo sasa.
Mkapa, ambaye alikuwa hakupangwa kuzungumza kwenye misa hiyo, aliombwa na mwongoza ibada ili atoe neno.
"Hali ya elimu ni mbaya na changamoto kubwa ni kufanya mageuzi kuanzia elimu ya msingi. Napata shida kuelewa watu wanapobadili madaraja ya ufaulu, tunakimbia nini," alihoji Mkapa.
Baada ya kutoa maoni yake, Mkapa alimmwagia sifa mume wa marehemu Alice, Joseph Rugumyamheto na kusema alikuwa mtendaji mahiri na mchapakazi katika Serikali ya Awamu ya Tatu.
Alisema akiwa Katibu Mkuu Utumishi, alifanikiwa kuleta mapinduzi katika Serikali ambayo hadi sasa matunda yake yanaendelea kuonekana.
Serikali kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Profesa Sifuni Mchome, ilitangaza viwango vipya ya ufaulu na kulifuta daraja sifuri, hali iliyoibua hisia tofauti kutoka kwa wadau wa elimu.
Wadau hao, wakiwemo Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, waliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kukamilisha mchakato wa viwango vipya vya alama za ufaulu elimu ya sekondari kwa kushirikisha wadau wa elimu kabla ya kuanza kutumika.
Mwenyekiti wa Kamati, Margareth Sitta, alisema mfumo huo mpya umepitishwa wakati mdau mkubwa, Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) halikushirikishwa.
Kutokana na maoni hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Philipo Mulugo, alipingana na katibu mkuu wake kuwa Serikali haijalifuta daraja sifuri. Chanzo: mtanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni