Ijumaa, 14 Februari 2014

ADHA YA WAATHIRIKA MAFURIKO WA MAGOLE-DUMILA NAMNA WALIVYOJIOKOA KWA VITI NA MEZA KWA KUSIMAMA ZAIDI YA MASAA MATATU KUNUSURI KIFO NA MAJI YA MAFURIKO MOROGORO.



Mwalimu Kongera.
Haya ndiyo sehemu ya makochi yaliyogeuka kuwa mwokozi kwa watu zaidi ya 20 kunusuru maisha yao ikiwemo na viti kwa kusimama zaidi ya masaa 3.

Na Mtanda Blog, Morogoro.
TULISIMAMA juu ya makochi zaidi ya watu 25 kwa muda wa masaa manne tukiwa na watoto wadogo wa miaka mitano hadi saba waliosimama juu ya mabega ya mama zao katika chumba kilichojaa maji ya mafuriko na ilifikia wakati tukawa tumechoka.



Lakini, tunashukuru mungu maji yalipungua taratibu kwa masaa mawili yakitoka urefu wa futi nane na yalipongua kwa urefu wa futi nne kulipata afueni maana tayari tulikuwa tumechoka na ingezidi saa moja mbele yetu, pale ndani hakuna angekuwa mzima.

Ilikuwa siku yenye mateso makubwa na uchungu wa kupotelewa na mali mbalimbali hasa kwa wale wananchi wa kijiji cha Magole ambao walizingirwa na maji ya mafuriko, licha ya kupotelewa na kila kitu, kwanza kila mtu alikuwa na aina yake ya kujiokoa kwani wapo niliowaona wapo juu ya miti ilimradi tu ni namna gani ya kutafuta njia ya kujinusuru na roho yake isipotee katika janga la maji ya mafuriko yaliyoambatana na kila aina ya uchafu.
Mwalimu wa shule ya msingi kijiji cha Magole wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro, Marthin Kongera (42) anaeleza mkasa mzima uliyoikumba familia yake pamoja na yeye mwenyewe na majirani waliokimbilia katika nyumba yake iliyojengwa na matofali ya saruji yenye vyumba viwili na ukumbi mmoja ili kuweza kujihifadhi na mafuriko yaliyoikumba tarafa ya Magole januari 22 mwaka huu majira ya saa 12 asubuhi.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya maalum katika nyumba za shule ya msingi Magole, Kongera anasema kuwa ilikuwa siku ya jumanne yeye na familia yake waliamka salama salimini majira ya saa 12 asubuhi na baada ya muda mchache akijiandaa kwenda kazi (shule mita 40 tu kutoka nyumbani kwake) alianza kuona maji yakitiririka huku yakiwa yamesomba uchafu na kadiri muda ulivyozidi kusogea mbele maji yao yaliendelea kufika eneo la shule na kuanza kusambaa sehemu kubwa.


Maji hayo yalielekea kwa kusambaa kwa kasi katika mitaa ya kijiji hicho ambacho mafuriko hayo yalitengenisha wakazi wa Bwawani na Magengeni na barabara yenye mwinuko mkubwa na kujikuta wakazi wa Bwawani wakiathirika zaidi na mafuriko hayo kutokana na maji kushindwa kuondoka na kutuwama kwa muda mrefu.

“Ni miujiza tu ya mwenyezi mungu kwani kama hakupenda uage dunia katika janga fulani ndivyo ilivyotokea kwetu sisi na kama mwenyezi mungu angependa tuage dunia katika mafuriko haya basi katika nyumba yangu wangeopoa maiti 25 ya watu wazima na watoto”. Alisema Kongera.


Mwenyezi mungu ndiye anayepanga kila jambo kwa kiumbe wake hivi ndivyo ilivyotokea kwao kwani kuokoka kwao na kifo cha maji ya mafuriko ni miujiza yake yeye pekee.

Baada ya familia ya mwalimu huyo kuzingirwa na maji hayo walishindwa kuyakimbia ikiwa ni mita 70 tu kufika nchi kavu na muda mchache aliwaona kundi la majirani zake wakihema na watoto wao wamewabeba wakielekea katika nyumba yake ili waweza kukaa kutokana na kile walichohofia nyumba zao zilizojengwa kwa matofali ya kuchoma ambayo walihisi zisingeweza kuhimili mihimili ya maji hayo.


Kongera alisema kuwa baada ya maji kuzidi na hakuna pa kukimbilia yeye pamoja na familia yake na wale majirani zake alichukua uamuzi wa kuingia nao ndani ya nyumba hiyo na kufunga milango na madirisha kisha kuwaamuru akinamama wasimame juu ya makochi na meza na watoto kusimama juu ya mabega ya mama zao huku wakiwa wameshikilia nondo za madirisha kwa muda wa zaidi ya masaa 4 kwani hali hiyo lilisaidia kidogo kuokoa maisha yao.

“Kiujumla kila aliyekuwa mule ndani alichoka sana hebu mwandishi fikiria kusimama sehemu moja tena katika kochi na meza kwa zaidi ya masaa 4 huku wengine wakiwa na watoto wa miaka mitano hadi saba wamesimama juu ya mabega yao, kama lingezidi saa moja au mbili yele maji kupungua hali ingekuwa mbaya ni lazima wangechukua maiti 25 katika nyumba yangu achia mbali sehemu nyingine”. Alisema mwalimu huyo.

Alisema kuwa kilichowaokoa ni kupungua kwa maji hayo ya mafuriko kufuatia maamuzi wa serikali wa kubomoa sehemu ya barabara na kuruhusu maji yaliyotuwama kwa masaa kadhaa kupungua na kuwapa afueni wao na wananchi wengine waliokuwa wamepanda juu ya miti, mapaa ya nyumba na juu ya dali za nyumba zao ikiwa njia mojawapo ya kujikoa.

Siku ya tukio baadhi ya wananchi walioathirika zaidi na mafuriko hayo yalishinikiza uongozi wa serikali ya kijiji kutoa ruksa ya vijana kubomoa sehemu ya barabara hiyo ili kutoa nafasi ya maji yaliyotuwama kupungua ili watu walioshindikana kuokolewa hasa wale waliopanda juu ya miti, paa za nyumba na dali za nyumba waweze kujiokoa kwani baadhi ya watu hao wengine walikuwa wakisikika wakiomba msaada lakini walishindwa kuwaokoa kutokana na waogeleaji kuwa wachache.


Fatuma Abdallah Funge (62) anaelezea namna alivyojikoa katika mafuriko hayo kuwa bila msaada wa vijana kumwokoa basi yeye angekuwa mmoja wa watu ambao wangepoteza maisha lakini anamshukuru mwenyezi mungu kumnusuru na kifo.


“Nawashuru vijana wawili ambao waliogelea na kufanikiwa kufika nyumbani kwangu na kunibeba ili kunipeleka nchi kavu lakini juhudi zao zilishindikana baada ya wenyewe kuchoka na kuamua kunipandisha juu ya mti eneo la shule ya msingi Magole hapo ndipo palikuwa na kazi kubwa ya kunipandisha”.

Alisema Bi Fatuma aliongeza kuwa alisikia karaha sana wakati akipandishwa juu ya mti hali hiyo ilitokana nay eye kushindwa kupanda kutokana na uzee hivyo mmoja alitangulia juu ya mti huo na kumshika mkono na mungine aliyesimama chini kumshika mwili na kufanikiwa kumpandisha juu tawi la mtu ikiwa ni umbali wa futi 9 kutoka ardhini.

Alisema kuwa wakati akiwa kule juu mti alipatwa na baridi kali na mwili mzima kuuma na baada ya maji hayo ya mafuriko kupungua yaliyodumu kwa zaidi ya masaa manne mpaka maji yalipopungua na vijana hao kufanya kazi tena ya kumshuka kutoka juu ya mti huo.


“Niliwaona wenzangu wamepanda juu ya miti hii ya hapa shuleni zaidi ya 30 nashukuru kuwa miti hii imekuwa mwokozi katika mafuriko haya kwani”. Alisema bibi huyo.


Mbali ya wananchi kupoteza mali katika janga hilo ofisi za kijamii ikiwemo shule, mahakama na ofisi za kijiji na kata ni miongoni mwa thamani zilizosomba pengine zingine kuharibika pamoja na nyumba za ibada ukiwemo msikiti kuu ijumaa Magole kushindwa kutumika kwa ibada ya ijumaa baada ya kujaa tope.


Kwa sasa bibi huyo analazimika kutembea kwa mkongojo baada ya maumivu yaliyotokana na kupandishwa juu ya mti hasa wakati akishushwa na kukosa nguvu kwania alitumia nguvu nyingi wakati akipandwa na kushusha katika harakati za kujikoa kifo cha mafuriko hayo.

Licha ya Mwalimu Marthin Kongera na Fatuma Abdallah Funge (62) kunusurika kifo kwa kujikoa kwa kupanda juu ya mti na kukaa chumba kilichojaa maji kwa masaa manne kwa mkazi wa kijiji hicho Shida Abdallah (24) yeye anakumbuka namna alivyonusurika kifo kwa kusombwa na maji ya mafuriko kwa umbali wa mita 350 kabla ya kufanikiwa kuparamia mti na kupanda na kukaa kwa zaidi ya masaa 12.


Akiongea juu ya mkasa wake Abdallah alisema yeye akiwa shambani akilinda mazao kama miwa, mahindi na minasi akiwa amelala usiku wa januari 21 majira ya saa 8 usiku alistushwa na ubaridi wa maji mwilini mwake akiwa amelala usingizi katika kipanda chake na baada ya kutaharuki alijikuta akiviringishwa na maji yenye kasi na kupelekwa sehemu asiyoijua.

Abdallah alisema kuwa baada ya kumtokea hali hiyo hakuwa na namna ya kujiokoa kwani hakuweza kuona sehemu ya kukimbilia licha ya kuwa na giza nene hivyo maji hayo yalimpeleka seheme asiyoitaka na kumpeleka katika mti na kujaribu kushika lakini hakuweza kufanikiwa kuukamata.


“Yale maji yalinistukiza na nilikuwa nimelala usingizi na baada ya kunisomba yalinipeleka umbali mrefu, sehemu nisiyoijua lakini yakanileka katika mti wa kwanza na kunizungusha na nilipojaribu kuushika nikashindwa na kunipeleka mti wa pili yakanizungusha hapo kufanikiwa kushika tawi na kuling’ang’ania na kufanikiwa kuupanda mti huo na kukaa juu kwa zaidi ya masaa 12 bila nguo zilizotokana na heka heka za mafuriko hayo”. Alisema Abdallah.

Mhanga huyu aliongeza kwa kusema kuwa alikaa juu ya mti huo kuanzia saa 8 usiku hadi asubuhi huku akijisikia baridi kali akiwa mtupu kama alivyozaliwa baada ya nguo zake kusombwa na maji na majira ya saa 9 alasiri ndiyo waokoaji walipofanikiwa kumwokoa huku akiwa amechoka na mtu aliyeonekana akili kutokuwa sawa.


Fadhil Masanzanzia (32) ndiye kijana aliyeongoza kujitosa katika maji ya mafuriko kupiga mbizi na mwenzake Hassan Rajab na Sud Alfan Sud kuongoza msafara wa waokoaji kufuata Shida Abdallah kwa lengo la kumwokoa wanaeleza ugumu wa kazi hiyo.

Masanzanzia anasema kuwa haikuwa kazi rahisi kumfikia, Shida Abdallah kutokana na kukumbana na vikwazo vingi ndani ya maji hayo ikiwemo kujigonga mwilini na mawe, magogo na maji kuwa mazito hali iliyolekea kuwa na ugumu wa uokoaji wa watu waliokwama juu ya miti mbalimba hasa katika upande ambao ulikumbwa zaidi na mafuriko hayo.


“Kikundi chetu kilikuwa na wapiga mbizi 18 lakini watu ambao tulikuwa mstari wa mbele na uwezo wa kuwafikia wahanga tulikuwa hatuzidi watano na tunashukuru tumefanikiwa kuwaokoa watu zaidi ya saba kutoka juu ya miti na kuwafikisha nchi kavu tukitumia madumu matupu ya ujazo wa lita 20”. Alisema Masanzanzia.


Katika hilo mwanzo ilikuonekana kazi ya kuwaokoa watu waliokwama katika miti ilionekana ni yakujitolea lakini tunamshukuru sana naibu waziri wa ujenzi na kuthamani juhudi zao na kutoa pesa sh40,000 akifuatiwa na mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera aliyetoa sh25,000 na kaka wa Hatibu Bakari, Makongoro Bakari kutoa kiasi cha sh10,000 baada ya kumwokoa ndugu yake na waogeleaji hao.


Afisa Mtenda wa kijiji cha Magole kilichopo tarafa hiyo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Hussein Nyongo anasema sehemu kubwa ya waathirika wa mafuriko hayo katika kijiji hicho ni wale wa mtaa wa Bwawani kutokana na eneo hilo kuwa ndiyo sehemu kubwa yaliyoanzia huku kukichangiwa na kingo za tuta kubwa la barabara iliyosababisha makaravati kuziba uchafu na maji kutuwama.


Kijiji hicho cha Magole kina mitaa sita lakini wananchi wake walioathirika zaidi ni wale wa mitaa ya Bwawani, Kichangani, Manyata na Zizini huku wale wa mitaa ya Magengeni na Mjimkuu wananchi wake wakiathirika kidogo.


Manyongo alisema kuwa tathimini iliyofanyika katika kijiji cha Magole inaonyesha kuwa jumla ya kaya zilizoathirika katika mafuriko hayo ni 1446 huku nyumba zilizobomoka zikiwa 290.


Ni mtu mmoja tu aliyeripotiwa kupotea aliyetambulika kwa jina la Mwesongo aliyekadiliwa kuwa na umri wa miaka kuanzia 55-60 huku mifugo ilisombwa na maji ni pamoja na ng’ombe mmoja, mbuzi 10, kuku 2370, bata 620, mahindi gunia 2970, mpunga 673, na thamani mbalimbali ya vyombo vya ndani na mavazi.


Vingine ni mchele kilo 185, alizeti gunia nne na kufanya mafuriko hayo kufanya iwe na wahanga 7230 katika kijiji hicho cha Magole pekee ambapo yanahitajika mahema 725 alisema Afisa Mtendaji wa kijiji cha Magole. Hussein Nyongo huku tathimini ya maeneo mengine yaliyokumbwa na mafuriko hayo ikiwemo, Mateteni, Mbigiri, Mabana na Kituo cha Elimu Dakawa zikiwa hajapatika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni