WARIOBA AMSHUKIA Prof SHIVJI, ASEMA CHANZO NDIYE YEYE CHA UCHOCHEZI ZANZIBAR.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa gazeti hili,
nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin
Mjwahuzi.
DAR ES SALAAM.
MJADALA wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya
Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa
Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya
Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye mwanzilishi wa
chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo ambalo sasa analigeuka
kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa
Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana
lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo lililokuwa na
dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano Baada ya Miaka 50.
Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es
salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo,
Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia
mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni Zanzibar,
Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika pande hizo mbili za
Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa viongozi
halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar,
Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa Tanzania ambao
hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa Shivji,
ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia
sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba walikuwa hawana
nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema
“the road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya kuzimu
imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema
Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar
na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa
matumizi ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwake
jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa
intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa
makusudi.”
Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa
chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema
waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa
Zanzibar.
“Shivji alikuwa anasema Tanganyika
imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi
isijifiche,” alisema Jaji Warioba.MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni