Jumanne, 18 Machi 2014
WAZIRI MKUU MSTAAFU MHE SUMAYE AKATA RUFAA
DODOMA.
Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amekata rufaa Kamati Kuu ya CCM kupinga adhabu ya onyo kali aliyopewa na chama chake kutokana na madai ya kuanza kampeni za urais mapema kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao. Akizungumza na gazeti hili mjini Dodoma hivi karibuni, Mhe Sumaye alisema kwa ufupi hakuridhishwa na adhabu hiyo na kuthibitisha hilo kuwa tayari amekata rufaa.
Hata hivyo, alisema hadi jana alikuwa hajapata mrejesho wowote kwa sababu kanuni hazielezi ni muda gani anatakiwa kuwa amepewa taarifa kuhusu rufaa hiyo.
Sumaye na wanachama wenzake, Edward Lowassa, Bernard Membe, Stephen Wassira, William Ngeleja na January Makamba walitiwa hatiani kwa kuanza kampeni mapema, hivyo kupewa onyo linalokwenda sambamba na kutowania nafasi yoyote ndani ya chama kwa miezi 12.
“Siwezi kuwazungumzia wenzangu, nazungumza kwa upande wangu, sikuridhishwa na adhabu hii na nimeshakata rufaa ingawa sijapata majibu yoyote, naendelea kusubiri,” alieleza Sumaye.
Waziri Sumaye alikataa kuzungumzia hali ya utekelezaji wa adhabu hiyo, akisema anachosubiri ni majibu ya rufaa yake aliyoiwasilisha Kamati Kuu ya CCM, mwanzoni mwa mwezi huu. “Sina kumbukumbu nzuri ilikuwa tarehe ngapi, lakini ni mwezi huu wa tatu.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa juu ya rufaa hiyo alisema hana taarifa zaidi ya kuzisikia kutoka kwa mwandishi.
Hata alipotakiwa kueleza nani anatakiwa kuwa na taarifa hizo, alisema: “Mimi ndiye msemaji wa chama, hakuna wa kuzungumzia suala hili zaidi yangu. Kwanza inatakiwa ijulikane, rufaa hiyo imepelekwa ngazi gani ya uongozi kwa sababu kila ngazi ina muda tofauti wa kufanya vikao vyake vya uamuzi.”
Nnauye baada ya kuelezwa kuwa rufaa ya Sumaye imewasilishwa Kamati Kuu ya CCM, alisisitiza kuwa hana taarifa nayo na kwamba haiwezekani rufaa ipelekwe kwenye kikao kilichotoa adhabu husika.
Hata hivyo, Sumaye alisisitiza kuwa rufaa yake ameiwasilisha Kamati Kuu kwa mujibu wa kanuni zinazohusika. MWANANCHI
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni