OGOPA TAPELI: WATU WATAPELIWA DAR
Advera Senso – SSP.
WATU zaidi ya 10 wametapeliwa fedha walizotuma kwa mtandao baada ya kurubuniwa kuwa wangepata mikopo katika taasisi, iliyojitambulisha kwa jina la Savings
Foundation Loans na kudai ofisi zake ziko katika Jengo la Utumishi. Wanadaiwa kutoa kati ya Sh 50,000 na 100,000 kwa watu hao,
wanaodaiwa ni matapeli, wakitumia jina la Menejimenti ya Utumishi wa Umma Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Florence
Temba alimwambia mwandishi watu waliotapeliwa, wamekuwa wakifika ofisini hapo
kufuatilia mikopo hiyo.
Kwa mujibu wa Temba, miongoni mwa waliotapeliwa,
wamo wakazi wa mikoa mbalimbali nchini, ambao wamekuwa wakipiga simu, kuulizia
mikopo hiyo baada ya kutakiwa na watu hao kutoa fedha.
Taasisi hiyo ya
kitapeli, ilielekeza watu kuwa makao makuu yake yako Dar es Salaam, Jengo Kuu la
Utumishi wa Umma “Ofisi ya Rais” kitengo cha Mikopo na Uwekezaji, Jengo Namba
360, ghorofa namba moja Customer Service fund.
Temba ambaye ofisi yake
jana ilitoa rai kwa vyombo vya habari, kuonya wananchi juu ya utapeli huo,
alisema hiyo ni mara ya pili kuhadharisha, lakini wamekuwa wakipokea maswali
kutoka kwa wananchi huku taasisi hiyo ikiendelea kuwatapeli kwa kutoa namba
zaidi kwa ajili ya kutuma fedha.
Wakati huo huo, polisi imesema utapeli
unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi na mtandao wa intaneti, umeenea nchini na
kutaka wananchi kuuliza kabla ya kuamua kufanya jambo lolote.
Msemaji wa
Jeshi hilo, Advera Senso aliliambia gazeti hili jana Dar es Salaam kwamba
matapeli hao, wamekuwa wakitangaza vitu ambavyo havipo kiuhalisia na kuwafanya
wananchi kuingia katika mkumbo.
Senso alisema hayo kutokana na hadhari
ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa wananchi dhidi ya utapeli,
unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi na mtandao wa intaneti.
TCRA
imetaka wanajamii kutokutoa simu wala kadi ya simu kwa mtu wasiyemfahamu. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, mmiliki
yoyote wa simu, asitoe maelezo yoyote kuhusu namba ya simu au taarifa za binafsi
kwa mtu. (TK)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni