Mume wa mwanamke aliyehukumiwa kifo nchini Suudan kwa kosa la
kuasi dini ya kiisilamu, ameambia BBC kuwa hajafahamishwa kuhusu mpango wa
kumwachilia mkewe.
Ripoti zilizotolewa Jumamosi ziliarifu kwamba afisa mmoja wa serikali
alithibitisha Meriam Ibrahim, aliyejifungua mtoto akiwa kizuizini ataachiliwa
katika siku chache zijazo.Taarifa za hukumu ya kifo iliyotolewa kwa mwanamke huyo, zimeikera sana jamii ya kimataifa.
Alikataa kusilimu na kusema kuwa yeye ni mkristo na hivyo anakabiliwa na hukumu ya kunyongwa kwa kosa la kuasi dini.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Sudan, Abdullahi al-Azreg, aliambia BBC Jumamosi kwamba, Bi Ibahim ataachiliwa huru kwani serikali ya Sudan inawapa watu uhuru wa kuabudu na hivyo iko tayari kumlinda.
Mumewe Meriam Daniel Wami, alisema kuwa taarifa za mkewe kuachiliwa ambazo amezisikia kupitia vyombo vya habari, ni kama uvumi tu.
“Hakuna afisa yeyote wa serikali amewasiliana nami. Labda kuna mashauriano kati ya serikali na maafisa wa kigeni, ikiwa ni hivyo taarifa hizo mimi sina,’’ alisema Daniel.
“Mimi nitasubiri tu kesi ya rufaa ambayo mawakili wamewasilisha, na ninatamani kuwa mke wangu ataachiwa huru.’’ BBC
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni