Viongozi wanaounda kundi la Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKawa). Kutoka kushoto, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba, Samuel Sitta, kwa kushirikiana na Makamu Mwenyekiti, Samia Hassan
Suluhu, wameteua wajumbe 30 wa Bunge hilo watakaoshiriki katika kikao cha kamati
ya Mashauriano kitafachofanyika Julai 24 na 25 mwaka huu, katika ofisi ndogo za
bunge jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya
habari jana na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis, wajumbe wa kamati hiyo
watafanya kazi ya kutathmini kazi ya bunge lao iliyokwisha kufanyika awali
pamoja na ile itakayofanyika mwezi ujao.
Alisema uteuzi huo umefanyika
chini ya masharti ya kanuni 54(4) na (5) za mwaka 2014.Aliwataja wajumbe
walioteuliwa katika kamati hiyo kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa muda
wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, Profesa Costa Ricky Mahalu, James Mbatia,
Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba, Peter Kuga Mziray, Vuai Ali Vuai, Askofu Donald
Mtetemela, Sheikh Thabit Norman Jongo, na Job Ndugai.
Wengine ni
Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema, Amon Anastaz Mpanju, Dk
Francis Michael, Tundu Lissu, Margareth Abdallah, Kidawa Hamid
Saleh,
Shamsi Vuai Nahodha, Abubakar Khamis Bakari, Dk. Asha Rose Migiro,
na Othman Masoud Othman.Kadhalika, yupo Stephen Wasira, Hamad Rashid Mohamed,
Askofu Amos Muhagachi, Susan Lyimo, Sheikh Hamid Masoud Jongo, Anne Kilango
Malecela, Mary Pius Chatanda, Profesa Mark Mwandosya, Magdalena Sakaya na
Khalifa Suleiman Khalifa.
CHIMBUKO LA MGOGORO
Aprili 16, mwaka
huu wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliusia
kikao cha Bunge hilo kwa madai ya upendeleo na ubaguzi uliokuwa unafanywa na
Chama Cha Mapinduzi dhidi ya vyama vingine.
Wajumbe hao wanaounda umoja
huo kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na wa vyama vingine, walichukua
hatua hiyo pia wakituhumu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, waliyodai kuwa ni za ubaguzi na vitisho akiwa
kanisani kwamba Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe
nchi ya Kiislamu.
Msimamo huo ulitolewa siku hiyo jioni na Profesa
Ibrahim Lipumba alisema kuwa Lukuvi alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma katika
Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa
Jimbo la Dodoma.
Profesa Lipumba alisema kwamba Lukuvi aliyemwakiisha
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumza lugha ya vitisho ndani ya kanisa kwamba
kama serikali tatu zitaundwa na serikali ya Muungano ikashindwa kuwalipa
mshahara wanajeshi, Jeshi litachukua nchi.
Alisema kuwa kauli hizo
zilisababisha Askofu Bundara kusema kwamba ni vema Katiba ya Zanzibar ikafutwa
na kuundwa katiba moja.
Lipumba alisema Bunge limegeuka kuwa Interahamwe
akimaanisha wanamgambo waliochochea ubaguzi na kusababisha mauaji ya kimbari
nchini Rwanda mwaka 1994.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini ya
dini ya mwenyezi Mungu, lakini naafiki mapendekezo yaliyoletwa kwetu na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ambayo ni Tume iliyoundwa na
Rais.
UBAGUZI.
“Na waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda…Mheshimiwa hii inasikitisha na inasikitisha kwa kuwa kauli
hii pia inafanana na kauli ambayo Rais Jakaya Kikwete aliitoa wakati akitoa
hotuba katika bunge hili,” alisema.
“Hii ni Rasimu ya Tume ya Rais na si
rasimu ya Wapemba, lakini katika mjadala wetu hapa umekuwa na utaratibu wa
ubaguzi, watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili
limekuwa kama Bunge la ‘Intarahamwe’, hii ni hatari kwa nchi yetu,
“Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo, hii hatuitaji katika nchi yetu,
tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake wote tuwe
sawa, bila kujali, rangi zetu, makabila yetu, dini zetu, hii ndiyo nchi
aliyotuachia Mwalimu Nyerere,” alisema.
“Kutokana na hali hii, tumechoka
kusikiliza matusi, tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi,
hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Interahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya
Tanzania…hili hatulikubali, hatulikubali, tunawaachia, watu wote tunaotaka
katiba ya wananchi tunawaachia Interahamwe muendelee na kikao chenu,”
alisema.
“Hatuwezi kuwa sehemu ya Interahamwe,” alisema Profesa Lipumba
na baada ya kumaliza kuzungumza, wajumbe wote wa Ukawa na wengine walisimama na
kuondoka ndani ya ukumbi huku wakipiga kelele.
Baada ya kutoka nje ya
ukumbi wa Bunge huku wajumbe wa kundi hilo linalojumuisha vyama vya hivyo pamoja
na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, DP kinachoongozwa na Mchungaji
Christopher Mtikila na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201, huku wakiimba nyimbo
mbalimbali. “Tunaondoka, tunawaacha Interahamwe, Interahamwe.”
LUKUVI
NA KANISA
Alitaja sababu nyingine iliyowafanya watoke nje ya ukumbi wa
Bunge wakati mjadala ukiendelea ni hatua ya Lukuvi kuzungumza ndani ya kanisa,
akieleza kuwa ulikuwa ni makakti maalum wa kuwabana Wazanzibari.
Profesa
Lipumba aliwataka wajumbe hao kuhudhuria kikao cha pamoja kitakachofanyika leo
kwa ajili ya kuweka mikakati ya nini cha kufanya.
TUTARUDI
IWAPO…
Baada ya kikao hicho, Prof. Lipumba alipoulizwa na waandishi wa habari
kama Ukawa wamesusia moja kwa moja Bunge la Katiba, alisema wanaweza kurudi
endapo tu mambo yatakayokuwa yakijadiliwa ni yale tu yaliyomo katika Rasimu
iliyopendekezwa na Tume ukiwamo muundo wa Muungano wa serikali
tatu.
MADHARA KWA THELUTHI MBILI
Ikiwa hawatarejea bungeni wataathiri
upitishaji wa katiba kwa sababu kanuni namba 36 (1) bila kuathiri masharti ya
sheria na kanuni hizi, mapendekezo ya marekebisho, au mabadiliko yaliokidhi
matakwa ya na masharti ya kanuni hizi kuhusu sura za rasimu ya katiba
zinazohusika yatajadiliwa na kupigiwa kura ibara kwa ibara katika kipindi
kisichozidi siku moja.
Ibara ya 2 inasema mapendekezo ya marekebisho au
mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasiri ya (1) yatapigiwa kura na
kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka
Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania
Zanzibar.
Ibara ya 3 inasema pale mapendekezo ya marekebisho, maboresho
au mabadiliko yatakubaliwa, ibara inayohusika ya rasimu ya katiba itahesabiwa
kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake isipokuwa kwamba pale ambako
mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yatakataliwa, ibara
inayohusika ya rasimu ya katiba itapigiwa kama ilivyokuwa kwa kufuata masharti
ya fasiri ya (2).
Ibara ya Nne, endapo baada ya kupigiwa kura, theluthi
mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote
kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye kamati
ya mashauriano ili kupata muafaka.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
inawatambua wajumbe wote waliokula kiapo na ndiyo sababu baadhi ya kamati
miongoni mwa 12, zilizochambua rasimu zilishindwa kupitisha maamuzi kutokana na
kukosa theluthi kwa pande zote wakati wa kupiga kura kutokana na baadhi ya
wajumbe kutokuwapo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni