Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho kilicho tokea siku ya Jumapili tarehe kumi mwezi huu kwa niaba ya mganga mkuu wa wilaya ya Ikungi daktari Philipo Kitundu ,amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa mtendaji wa kata ya Iyumbu walifika kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa awali na walikuta marehemu ambaye ametambulika kwa jina la Jibulu Mahende akiwa amekufa ndani ya duka la kuuzia dawa.
Baada ya kufanya uchunguzi daktari Kitundu walibaini kuwa marehemu alikufa wakati akipitiwa matibabu na bwana Prosper Simson ambaye hana taaluma ya udaktari kwa kumwongezea maji chupa tisa yakiwa na dawa ambazo hazikufahamika mara moja na vidonge sita ambavyo pia havijafahamika, pia walibaini kuwa bwana Prosper Simson hakuwa na leseni kutoka TFDA ya kufanya biashara hiyo na yeye mwenyewe hana cheti chochote alicho somea taaluma ya udaktari.
Kwa upande wake bwana Prosper Simson ambaye anajifanya daktari amekiri kumpokea bwana Jibulu Mahende ambaye kwa sasa ni marehemu na kusema kuwa awali alikuwa akitibiwa kwa waganga wa jadi na alikuwa akisumbuliwa na kifua na kumshauri aende kutibiwa katika hospitali ya mkoa wa Singida au hospitali ya Itigi.
Mtoto wa marehemu bwana Jilala Jibulu ambaye alifuatana na baba yake amesema baada ya mgonjwa kuwekewa chupa za maji aliondoka na kwenda kutafuta hela za kumpeleka baba yake katika hospital ya mkoa wa Singida ambayo ipo kilomita 140 kutoka katika kijiji cha Iyumbu, na baada ya muda alipigiwa simu na kuambiwa kuwa baba yake alikuwa amekwishafariki.
Jeshi la polisi limefika katika kijiji cha Iyumbu na kumshikilia bwana Prosper Simson ambaye anajifanya daktari kwa uchunguzi zaidi.
CHANZO: EATV
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni