Jumatano, 1 Oktoba 2014
POLISI ACHUNGUZWA NA POLISI KISA KUTOROSHA DENT
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Moita Koka
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linachunguza tukio la askari wake (jina tunalo), iwapo alimtorosha na kumweka kinyumba mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Okaoni, wilayani Moshi Vijijini.
Askari huyo anatuhumiwa kumrubuni mwanafunzi huyo kuwa atamnunulia magauni mawili, blauzi mbili, sketi mbili pamoja na kiasi cha Sh 100,000.
Pamoja na kumtorosha mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, askari huyo na mwanafunzi, walipata ajali ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kutoka mjini Moshi kwenda Kibosho, Septemba 27 majira ya saa 9 alasiri na kulazwa hospitali ya KCMC na baadaye Kibosho Hospitali.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Moita Koka alithibitisha kupata taarifa za askari huyo na tuhuma dhidi yake na kuongeza kwamba maofisa wake wameanza kuchunguza tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa pale itakapothibitika.
“Hata mimi nasikia taarifa hizo za askari kumtorosha mwanafunzi na kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini hilo siwezi kulizungumzia maana halijathibitika, nimetuma maofisa wangu wachunguze wakinipa taarifa nitatoa,” alisema.
Aidha, Kamanda Koka alisema taarifa alizonazo ni juu ya kupata ajali kwa askari wake akiwa amembeba msichana, lakini hajapewa taarifa kama msichana huyo ndiye mwanafunzi anayezungumziwa na kama kweli wana mahusiano ya kimapenzi ama la.
“Kwa ujumla hili tukio hasa upande wa mapenzi siwezi kulizungumzia, ninachofahamu na ambacho nimekitolea maelekezo ni kutaka kupewa taarifa za ajali inayozungumziwa... lakini hili la mahusiano nalo nimetaka nipewa taarifa zake, ikibainika sheria itachukua mkondo wake,” alisema.
Kwa upande wake, diwani wa kata ya Okaoni na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Moshi Vijijini, Moris Makoi, alithibitisha taarifa za askari kumtorosha mwanafunzi huyo na kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi.
Makoi alisema askari na mwanafunzi huyo pia walipata ajali eneo la Memorial barabara kuu ya Moshi/Arusha wakati wawili hao wakirejea Kibosho kutoka Moshi mjini walikokuwa wamejificha.
Naye mwanafunzi huyo, akiwa katika wodi namba tano hospitali ya Kibosho, alikiri kupewa ahadi ya kununuliwa nguo na Sh 100,000 ambazo hakupewa.
Alisema, baada ya kufika mjini Moshi alikwenda kununuliwa vitu hivyo na kwenda nyumba ya kufikia wageni ambako walikuwa na mahusiano ya kimapenzi na wakati wakirejea Kibosho wakiwa na pikipiki hiyo walipata ajali na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
“Wakati tunatoka mjini tulipata ajali na nilipoteza fahamu na majira ya usiku nilijikuta nimelazwa Hospitali ya KCMC na siku iliyofuata yule askari alikuja na kunichukua na kunirejesha nyumbani,” alisema.
Hata hivyo, mwanafunzi huyo alisema baada ya kufika nyumbani maumivu yaliendelea kuwa makali na kuamua kupelekwa katika hospitali ya Kibosho kuendelea na matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Kibosho, Erin Mmassele alikiri kumpokea mwanafunzi hayo na kuongeza kuwa anaendelea vizuri licha ya kuwa na majeraha miguuni.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni