Kundi
la Watanzania 26 limerejea nyumbani kutoka Afrika Kusini leo tarehe 25
Aprili, 2015 kufuatia mashambulizi ya wazawa dhidi ya wageni. Kundi
hilo la kwanza kurejea nyumbani liliwasili katika Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere saa 11 alfajiri na Ndege ya Fast
Jet.
Watanzania hao walikuwa wanaishi katika kambi za dharura
za Isipingo na Phoenix zilizopo jijini Durban. Walisindikizwa kurudi
nyumbani na Afisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw.
Elibahati Lowassa. Zoezi la kuwarejesha wananchi hao lilisimamiwa na
kuratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Wakati
huo huo, Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umepata taarifa kuwa
kuna Watanzania wengine wapatao 20 wanaishi kwenye Kambi ya Hillbrough
jijini Johannesburg. Ubalozi umetuma Afisa kwenda katika kambi hiyo ili
kufanya uhakiki wa taarifa hizo kwa madhumuni ya kuwarejesha nyumbani
Tanzania haraka iwezekanavyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
25 Aprili 2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni