Jumapili, 7 Juni 2015

KIGOGO WA IKULU ALIYEPATA MGAWO WA ESCROW AONDOLEWA

 

Mnikulu Shabani Gurumo, aliyepokea asante ya Shilingi milioni 80.8 katika mgawo wa fedha za kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, ametimuliwa Ikulu.


Taarifa za kuondolewa Gurumo, zilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, katika mahojiano na gazeti hili ambaye alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa wiki moja iliyopita.
Gurumo aliyekuwa na wadhifa wa Mnikulu Mkuu wa Ikulu, alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing James Rugemalira, alipohojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.

Rugemalira alikuwa mbia (mzawa) wa kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL ambayo pamoja na Tanesco zilifungua akaunti hiyo ya Escrow.

Fedha alizopokea Gurumo zinadaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilizochotwa kifisadi katika akaunti hiyo, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Balozi Sefue alisema hawana cha kumfanya kwa upande wao na kwamba Ofisi ya Utumishi wa Umma ndiyo yenye jukumu la kuamua kinachofuata dhidi ya mtumishi huyo. “Sisi hatuna cha kufanya zaidi ya kuondolewa Ikulu, Ofisi ya Utumishi itaamua nini kinachofuata.”

Awali Mnikulu huyo alipinga madai ya yeye kupewa zawadi hiyo ya Escrow lakini alikiri kuwa alipokea Shilingi milioni 80.8 kutoka kwa Rugemalira kwa sababu za urafiki walionao kwa muda wa miaka 10 na hazihusiani na mgawo.

Gurumo alieleza kuwa Rugemalira ni rafiki yake kwa muongo mzima na kwamba ndiye aliyemshauri kufungua akaunti kwenye Benki ya Biashara ya Mkombozi, tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumuingizia kiasi cha Shilingi 80, 850,000 katika akaunti hiyo.

Aliwaambia wajumbe wa Tume ya Maadili kuwa aliyemuunganisha na Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa hospitali binafsi ya Sanitas, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam.

Alijieleza zaidi kuwa hata siku moja hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na Rugemalira, mbali na ya kifedha na pia hana uhusiano wowote na kampuni ya VIP Engineering and Marketing.

Akasema anahisi pengine Rugemalira alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa na maradhi ya saratani.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ilitoa taarifa kuwa Shilingi bilioni 301 zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kusababisha vigogo kadhaa akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kujiuzulu.

Wengine waliopokea mgawo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alikiri kupokea shilingi bilioni 1.6, ambazo zilisababishwa kutimuliwa uwaziri.

Pamoja naye Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, naye akijiuzulu kwa kashfa hiyo iliyosimamiwa na wizara yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alipoulizwa kuhusu kutimuliwa ikulu kiongozi huyo na hatua gani zitakazochukuliwa alilitaka gazeti liwasiliane na Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Hab Mkwizu kwa ufafanuzi.

Hata hivyo, Mkwizu hakupatikana hadi gazeti hili lilipokwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni