Jumatatu, 15 Juni 2015

MUFTI MKUU SHEIKHE ISSA BIN SHABAAN SIMBA AFARIKI DUNIA KUZIKWA LEO SHINYANGA.

Mufti Simba enzi za Uhai wake.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, amefariki dunia alfajiri ya jana katika hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.


Taarifa kutoka mamlaka husika na dini na ndugu wa karibu walieleza kuwa, mwili wa marehemu umeondolewa hospitali hapo na kuhamishiwa hospitali kuu ya Jeshi ya Lugalo kungoja taratibu za mazishi.

Kwa mjibu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo pamoja na presha. Mwili wa marehemu utasafirishwa leo mkoani Shinyanga kwa ajili ya maziko yatakayofanyika leo mjini hapo.



Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.

 
إِنَّا للهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ‎)


Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara (Mb.) ametuma salamu za rambirambi kwa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (BAKWATA) na Waislamu wote nchini kufuatia kifo cha Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba kilichotokea Jumatatu, tarehe Juni 15,2015 katika hospitali ya TMJ Jijini Dar es Salaam alipokuwa anatibiwa.

Katika salamu hizo, Mhe. Mukangara amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kumpoteza kiongozi huyo ambaye bado Taifa lilikuwa likimuhitaji hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Waziri huyo ameongeza kuwa Mufti atakumbukwa kwa upole, unyenyekevu wake na kutopenda makuu, wakati wa uhai wake marehemu alikuwa tayari kumsikiliza kila mtu bila kujali dini au kabila lake.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya kifo cha Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba ambaye alikuwa Kiongozi anayeshirikiana vizuri na viongozi wote wa serikali na vyama mbalimbali katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa wamoja” amesema .

Amesema Waziri Mukangara: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi wewe Katibu Mkuu, BAKWATA na waislamu wote nchini na naungana nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu.

Aidha, kupitia BAKWATA, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu kwa kumpoteza mpendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke pema peponi roho ya marehemu … Amina.”

Imetolewa na: Idara ya Habari(MAELEZO)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni