Jumanne, 7 Januari 2014

BOTI YA MV KILIMANJARO II YAIBUA MAJONZI UPYA KWA WATUMIAJI WA USAFIRI WA MAJINI DAR ES SALAAM-ZANZIBAR.

Kwa masikitiko makubwa tunapokea taarifa nyingine za maafa ya usafiri baharini hii ni mara ya tatu kutokea maafa kama haya au yanayofanana na haya katika kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya Serikali ya Umoja wa kitaifa inayoongozwa na Dk Ali Mohammed Shein.

Maswali mengi yanaulizwa ikiwa ni pamoja na ni kwa nini Mamlaka zinazohusika haziwezi kuchukua hatua za dharura na za haraka inapotokea hatari kama hii? Jee watendaji na wenye kumiliki usafiri baharini nao wanakaguliwa na kuadhibiwa wanaposababisha maafa na kufanya uzembe kama huu? Jee Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa taarifa na kama inatoa jee wahusika wanapokiuka na wasipozingatia uhai wa wananchi wanyonge waachwe tu kila siku wakisababisha vifo vya watu?.

Hili ni wimbi kubwa lililosababisha dhoruba kwa meli husika

Kwa taarifa za kuaminika ni kwamba tayari miili ya watu watano imeshaokotwa ikiwa inaelea baharini baada ya chombo cha usafiri kilichokuwa kikitokea Pemba na kuelekea Unguja kilipofika katika mkondo wa Nungwi kikapigwa na dhoruba kali ya upepo na watu waliokuwa mbele ya boti hiyo ya Kilimanjaro 2 wakaingia baharini na kuzama hali ambayo ilileta mtafaruku mkubwa kwa abiria waliokuwemo ndani ya chombo hicho lakini pia kwa wananchi waliokuwepo majumbani wakipeana taarifa mbali mbali za maafa hayo na vifo huku wengine wakiwa na taharuki kubwa baada ya kujua ndugu na jamaa zao wamo ndani ya chombo hicho.

Kwa uchunguzi mdogo uliofanywa tokea asubuhi ilipotokea hitilafu Boti ya Kilimanjaro 2 ni kuwa kuna udhaifu fulani katika mamlaka zinazosimamia usafiri nchini kuanzia serikalini hadi kwa wamiliki wa boti hizo.

Maiti ni wawili wanawake na watatu wanaume kwa mujibu wa taarifa za sasa hivi kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Bw. Abdi Omar amesema usiku huu katika taarifa yake na waandishi wa habari huko Bandarini Malindi. Mkurugenzi anasema bado wataendelea kesho asubuhi kuwatafuta watu waliopotea baharini katika maeneo ya Nungwi.

Maiti wote wameletwa mjini kwa ajili ya kutambuliwa wapo katika hospitali ya Mnazi Mmoja baadaye serikali itaandaa utaratibu wa kawaida kwa maiti hizi kuzikwa ama kupewa jamaa zao.

Nahodha Nassor Abubakar Khamis ameshikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi anasema baada ya kupata hizo taarifa waliwahoji wahusika wa boti lakini Manahodha wa boti hiyo walisema hawajaona kama kuna watu wamepotea lakini wao waliona mizigo tu imeanguka.


Inasemekana kuwa jumla ya abiria 396 walisafiri na chombo hicho huku watoto wakiwa ni 60 lakini baada ya kufanya hesabu wakakuta idadi hiyo imepunguwa kuna watu kama 20 wamekosekana ndani ya chombo hicho na ndipo walipolazimika kufanya uchunguzi na kufuatilia huko Nungwi na kweli wamepata miili mitano na waliookolewa wakiwa hai ni watatu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni