PICHA|MAKTABA
Watu 10 wamefariki dunia na wengine 17 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea mikoa ya Pwani na Mwanza.Katika ajali ya mkoani Pwani, watu saba wamefariki dunia na wengine tisa wakiwa majeruhi baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori huko Chalinze Mzee, Barabara ya Chalinze - Segera wilayani Bagamoyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea saa mbili usiku wa Machi 4 na kwamba watu hao tisa hali zao ni mahututi.
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea Msata kwenda Dar es Salaam na lori ambalo lilikuwa likitokea Chalinze kwenda Tanga.
Aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Ismali Hussein, Ndege Ally, Tunu Said, Khalfan Hussein, Tumaini Hussein, Jaffar Selemani na Emmanuel David ambao miili yao ilihifadhiwa katika Kituo cha Afya Chalinze.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni kondakta wa basi hilo, Deo Moses, dereva wa lori, Shaban Omar; utingo wa lori, Shoshy Mohamed na mwanafunzi darasa la kwanza, Shule ya Msingi Kwaifugo Mkata, Abdul Wela. Wengine ni Bitela Msuha, Zaina Mkombozi, Salumu Idd, Chadugu Paulo, Geofrey Anthony na Juma Athuman. Majeruhi wengine majina yao hayakutambulika mara moja.
Alisema majeruhi wengi wa ajali hiyo wameumia vibaya baadhi wamevunjika miguu na mikono na wote walipelekwa Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu.
Hata hivyo, mashuhuda wa ajali hiyo, Hussein Khalfani na Yusufu Hussein walisema ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa basi hilo alipokuwa akijaribu kuyapita malori waliyokuwa mbele yake.
Mwanza
Watu watatu wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kugonga daraja na kupinduka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlohola alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 3:40 asubuhi katika Kijiji cha Ng’ombe wilayani Misungwi baada ya tairi la nyuma upande wa kulia wa gari hilo lililokuwa likitokea Mabuki kwenda Mwanza, kupasuka.
Alisema dereva wa gari hilo, Patric Peter (28) alifariki dunia pamoja na abiria wengine wawili, Makoye Nyanda (30) na Hawa Abel (25).
Aliwataja majeruhi kuwa ni Angelina Abel (24), Shija Kabuki (22), Bune Chenya (40) na Johari Malungu (24) ambao wote wamelazwa katika Hospital ya Rufaa ya Bugando.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni