Algeria imefuzu kwa raundi ya pili ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza katika historia.
The Desert Foxes walitoka nyuma bao moja kwa nunge dhidi ya Urusi katika kipindi cha kwanza na kusawazisha na hivyo kufuzu kama mshindi wa pili katika kundi H nyuma ya Ubeljiji. Hii ndiyo mara yao ya kwanza kupita mkondo wa kwanza.
Algeria itaingia katika kumbukumbu za historia ya Soka Afrika kuwa mwakilishi wa 6 kuwahi kufuzu kwa raundi hiyo ya 16 bora nyuma ya Cameroon Ghana Nigeria Morocco na Senegal .
Algeria ilikuwa imefungwa mapema katika kipindi cha kwanza kupitia kwa mkwaju wake Aleksandr Kokorin aliyepata pasi murua kutoka kwa Dmitri Kombarov.
Hata hivyo vijana wa kocha Fabio Capello walianza kulinda ngome yao mapema bila ya tahadhari kuwa bao lolote la Algeria ingewarejesha nyumbani.
Mashambulizi ya Algeria yalizaa matunda kunako dakika ya 60 Islam Slimani alipoisawazishia Algeria kutokana na mkwaju wa freekick uliopigwa na Yacine Brahimi.
Wadau watachunguza tukio ambalo shabiki mmoja anadaiwa kumulika kifaa cha Laser usoni mwa kipa wa Urusi Igor Akinfeev kabla ya bao hilo la kusawazisha.
Kocha Capello amelalamikia hatua ya refarii kupuuza tukio hilo akisema kuwa huenda marefarii wananjama ya kuihujumu timu ya Urusi.
Urusi ilifanya mashambulizi kwenye lango la Algeria lakini wapi safu ya ulinzi ilikaa ngangari na kuhimili mashambulizi hadi kipenga cha mwisho na hivyo kuipa Algeria alama moja muhimu iliyoiwezesha kuweka historia ya kufuzu kwa raundi ya pili ya kombe la dunia.
Algeria sasa imeratibiwa kukwaruzana na Ujerumani katika mechi ya 16 bora siku ya jumatatu.Chanzo BBC Swahili
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni