Alhamisi, 26 Juni 2014

CHINA KUNYONGA VIJANA 65 WA TZ KISA 'UNGA'

Vijana 65 wa Tanzania wamehukumiwa adhabu ya kifo nchini China baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Vijana hao ni kati ya zaidi ya 403 wa Tanzania wanaoshikiliwa katika nchi mbalimbali duniani kwa tuhuma ya kujihusisha na biashara hizo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. William Lukuvi, mjini Dodoma wakati akizungumzia Maadhimisho ya Siku Dawa za Kulevya Duniani yanayofanyika Juni 26 kila mwaka.

Mhe Lukuvi alisema kuwa kwa mwaka huu maadhimisho hayo, kitaifa yatafanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nzovwe jijini Mbeya na Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Tangu mwaka 2008 kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wenye asili ya Kitanzania kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi, mpaka hivi sasa idadi yao ni kubwa kiasi cha kufikia zaidi ya 400, na wanashikiliwa katika nchi mbalimbali ambazo pia adhabu zao zinatofautiana kulingana na sheria za nchi hizo,” alisema Lukuvi.

NCHI WANAKOSHIKILIWA
Alizitaja baadhi ya nchi ambako vijana hao wanashikiliwa kuwa ni Brazil (108), Hong Kong (118), Kenya (34), Pakistan (16) na China 65.

Nyingine ni Japan (7), Malawi (5), Uganda (3), Uswisi (2), Marekani (2), Uturuki (1), Botswana (5) na Msumbiji (1).
“Orodha ya nchi waliko vijana hao ni ndefu zaidi,” alisema.

Akizungumzia maadhimisho hayo kwa nchini, Mhe Lukuvi alisema kauli mbiu yake kwa mwaka huu ni ‘Uteja wa dawa za kulevya unazuilika na kutibika, chukua hatua'.

Alisema Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye tatizo kubwa la dawa za kulevya kulingana na takwimu za ukamataji wa dawa hizo.

Kwa mujibu wa Mhe Lukuvi, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu kiasi cha kilo 220 za dawa hizo aina ya Heroine na watuhumwa 18 walikamatwa huku pia kilo 15.4 za Cocaine zilikamatwa pamoja na watuhumiwa saba.

Mhe Lukuvi alisema kwa sasa dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa maendeleo ya taifa kwa sababu imethibitika kuwa matumizi yake hupunguza tija na ufanisi wa nguvu kazi ya taifa.

SHERIA MPYA YAJA

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imekamilisha muswada wa sheria mpya ya dawa za kulevya ambao kama utapitishwa bungeni na kuwa sheria kama ulivyo, unaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza tatizo hilo.

Mhe Lukuvi alisema tofauti na jinsi ilivyo sheria ya sasa, sheria mpya itaondoa adhabu ya faini na watuhumiwa kunyimwa dhamana wanapokamatwa, hali ambayo itasaidia kukabiliana na wasafirishaji na wauzaji wa dawa hizo.

Kwa mujibu wa Mhe Lukuvi, sheria hiyo itakwenda sambamba na uundaji wa chombo imara cha kushughulikia dawa za kulevya ambacho kitakuwa na uwezo wa kupeleleza, kukamata na kushitaki watuhumiwa wa dawa za kulevya kama ilivyo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Alisema kuwa muswada huo tayari umekamilika na kwamba wakati wowote unaweza kuwasilishwa bungeni ili upitishwe hatimaye kuwa sheria.

Alisema maadhimisho hayo pia yatafanyika katika ngazi ya mkoa nchini na kuwaomba wananchi kujitokeza kushiriki ili waweze kupata elimu ya kutosha juu ya madhara na vita dhidi ya dawa hizo.
KANDORO ANENA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amewataka wananchi mkoani mwake walioathirika na dawa za kulevya kujitokeza kwa wingi kupima afya zao, kupata tiba na ushauri katika maadhimisho hayo.

Kandoro alifafanua kuwa maadhimisho hayo yanafanyika mkoani humo kutokana na takwimu kuonyesha una kiwango kikubwa cha tatizo la dawa za kulevya kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na kutoa mfano wa bangi ambayo inalimwa kwa wingi.

“Kama mnavyojua, mkoa wetu upo mpakani hivyo tuna changamoto kubwa sana ya uingizaji wa dawa hizi, mara nyingi watu hukamatwa katika mipaka ya Tunduma na Kasumulo, hivyo ni budi elimu hii kutolewa kwa wananchi ili tushirikiane wote katika kushinda vita hii tuliyonayo,” alisema Kandoro.

Alisema kuwa pombe aina ya viroba vya bei nafuu vitokavyo Malawi ni changamoto pia kwani vijana wengi wanavitumia, hivyo kuathirika kwa kiasi kikubwa. (TK) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni