Tanga. Watu watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Kwasunga wilayani Handeni wamekufa baada ya kula futari ya mihogo inayosadikiwa kuwa na sumu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:00 usiku eneo la Kwasunga Handeni na maiti zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Kamanda Massawe aliwataja waliokufa kuwa ni Juma Jumbe (6), Abdi Jumbe (10) na Ramadhani Jumbe (15). Pia alisema kuwa wazazi wa watoto waliwahishwa hospitali ambako walipatiwa matibabu na wanaendelea vizuri.
Kamanda Massawe alisema kwa mujibu wa wazazi wa watoto hao, walikula futari hiyo na baada ya kumaliza, walianza kujihisi vibaya sambamba na kuishiwa nguvu na alianza kuanguka mmoja baada ya mwingine.
Kamanda huyo aliwataka wote walio katika mfungo kuichunguza mihogo wanayoinunua kwa ajili ya matumizi ya futari kwani baadhi haifai kuliwa na binadamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni