Mkurugenzi Huduma za Kibenki kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Boaz (wa kwanza kulia) akiwaeleza waandishi wa habari (Hawapo Pichani) sababu zilizopelekea kutoa toleo jipya la sarafu ya shilingi 500, ambapo noti hiyo ya shilingi 500 inatumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida ya kila siku hivyo hupita kwenye mikono ya watu wengi na kuchakaa haraka,noti hizi hukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki na sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa muda mrefu kuliko noti. Katikati ni Mshauri wa Fedha kutoka ofisi hiyo Bw. Hassan Jarufu na Mwisho ni Meneja Msaidizi, Sarafu Bw. Abdul Dola.
Mkurugenzi Huduma za Kibenki kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Boaz (kulia) na Mshauri wa Fedha kutoka ofisi hiyo Hassan Jarufu wakiwaonesha waandishi wa Habari(Hawapo Pichani) Toleo jipya la sarafu ya Shilingi 500 inayotarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko kuanzia mwezi Oktoba 2014.
Benki Kuu ya Tanzania imetoa toleo jipya la sarafu ya shilingi 500 itakayoanza kutumika Oktoba 2014 itakayokuwa mbadala wa Noti ya shilingi 500 inayoonekana kuchakaa haraka.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma za kibenki wa benki hiyo Bw. Emmanuel Boaz wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
“Noti ya shilingi 500 hupita kwenye mikono ya watu wengi zidi na ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida hivyo kuchakaa haraka ndio maana tumeamua kutoa toleo la sarafu itakayoanza kutumika mapema mwezi wa 10 mwaka huu.”alisema Boaz.
Akifafanua zaidi Boaz amesema Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti na pia noti zimekuwa zilikaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe.
Akitaja sifa za sarafu hiyo mpya Boaz amesema kwanza umbo lake ni la duara lenye michirizi pembezoni na kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5.
Sifa nyingineni kuwa ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma na Nickel na kwa upande wa mbele ina sura ya Rais wa kwanza wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.
Pia Boaz alibainisha kuwa sarafu hiyo kwa upande wa nyuma ina kivuli kilichojificha ambacho huonesha thamani ya sarafu ya 500 au neno BOT inapogeuzwa geuzwa.
Kwa upande wa matumizi Boaz amesema sarafu hiyo itakapoanza kutumika itatumika sambamba na noti za shilingi 500 hadi zitakapokwisha kwenye mzunguko.
Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini ambapo katika kutimiza jukumu hili Benki kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denomination) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni