KUIBUKA
kwa makundi ya vijana ya uhalifu Dar es Salaam, kumesababisha uongozi
wa mkoa kuanzisha daftari maalumu la kudumu la taarifa za wahalifu wote
wa jiji hilo, ikiwa ni harakati za kumaliza tatizo hilo.
Daftari
hilo ambalo litakuwa na kazi ya kutunza orodha ya wahalifu wote kuanzia
ngazi za mitaa, litasaidia kuwapata wahalifu kiurahisi watakapofanya
matukio katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki wakati akizungumza na waandishi
wa habari baada ya kuzindua mpango wa kunusuru kaya masikini wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) Awamu ya Tatu.
Akifafanua kuhusu kurahisisha
kuwapata wahalifu, kutokana na taarifa katika daftari hilo, Sadiki
alisema wahalifu watakaorodheshwa katika daftari hilo, kutakuwa na
taarifa zao kamili na makosa wanayotuhumiwa nayo, hivyo watakapofanya
makosa itajulikana ni akina nani.
“Tunaanzisha benki ya wahalifu
ambapo ndani ya daftari hilo kutakuwa na orodha yote ya wahalifu kwa
maana hiyo kama mtu kafanya uhalifu eneo fulani, itafuatiliwa kwenye
daftari na kujua ni wahalifu gani watakusanya na watakaokuwa hawana
hatia wataachiwa,” alisema Sadiki.
Alisema katika hilo,
hakutakuwa na uonevu wa aina yoyote kwa mtu yeyote, bali watafanya hivyo
kwa kufuata haki na sheria. Aidha, alisema madaftari hayo yatakuwepo
kuanzia ngazi ya chini ya mitaa hadi ofisi ya mkuu wa mkoa.
“Hapa leo tumezindua mpango
mzuri sana, lakini hata tuwe na mipango ya maendeleo mazuri kiasi gani
bila kuwa na amani ni sawa na bure, nawaomba chokochoko zozote
zinazoweza kuvunja amani tusizifumbie macho,” alisema.
Aliwataka madiwani
waliohudhuria mkutano huo, kuhakikisha wananchi wao wanaishi kwa usalama
na amani kwa kusaidia kushirikiana na vyombo vingine vya usalama,
ikiwemo kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa katika kudhibiti
makundi ya uhalifu.
“Kuna makundi ya vijana wahuni
kama hawa wanaojiita panya road, mbwa mwitu na mengine ya aina hiyo
hawa ni wahalifu, tushirikiane kudhibiti makundi haya kwa kutoa taarifa
hata kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na ofisi nyingine za serikali,”
alisema.
Aidha, Sadiki alionya tabia
iliyozuka ya vyama vya siasa kukataa matokeo ya uchaguzi kwa kufanya
vurugu. Alisema kufanya hivyo hakuimarishi demokrasia, bali ni
kuizorotesha na kuiua.
“Jana tulishuhudia vurugu
zilizotokea wakati wenyeviti wa mtaa wa Manispaa ya Kinondoni
wakiapishwa, kundi la watu liliibuka na kufanya vurugu, lilijeruhi watu
eti wanadai wanapinga wale wanaoapishwa, jamani mbona sheria iko wazi na
bahati nzuri kuna watu wanashikiliwa kutokana na tukio hilo,” alisema.
Alisema kama watu hao
hawakuridhika, walipaswa kufuata taratibu, ikiwemo kwenda mahakamani,
lakini demokrasia ya makonde haikubaliki. Alisema amemuagiza Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, kuwachukulia hatua waliofanya tukio hilo bila
kujali vyeo au vyama vyao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni