Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando amesema hatua iliyochukuliwa na uongozi wa KCMC ya kumsimamisha kazi mtumishi wa Idara ya Uhasibu, Paul Mhumba siyo sahihi.
Mhumba alisimamishwa kazi Mei 5, mwaka huu kwa madai ya kutuma ‘meseji’ kwa Rais Jakaya Kikwete akimweleza kuhusu ubadhirifu katika hospitali hiyo.
Hatua ya uongozi wa KCMC kumsimamisha kazi mtumishi huyo imeendelea kuibua maswali kwa watu wa kada mbalimbali kwamba imekuwaje ujumbe wa siri aliotumiwa Rais umeifikia taasisi hiyo pamoja na namba ya mtumiaji.
Wakati sintofahamu hiyo ikiendelea, Mhumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), Tawi la KCMC katika barua yake ya Mei 16 kwa Dk Mmbando, alimwomba afike kwa uongozi huo kutoa ushahidi.
Alimtaka awe shahidi wake baada ya uongozi huo kudai kuwa yeye ndiye aliyewapa ujumbe huo na namba ya mtumaji.
Hata hivyo, jana Dk Mmbando hakueleza chochote juu ya madai ya kuhusika na kutuma ujumbe huo kwa ‘meseji’ lakini alikosoa hatua iliyochukuliwa na uongozi wa KCMC kwa mtumishi huyo.
“Siyo sahihi kwa hatua waliyochukua KCMC. Kiongozi anapopewa taarifa zenye mapungufu kwenye taasisi ni kwa ajili ya kumsaidia kutatua changamoto hizo,” alisema Dk Mmbando.
Kuhusu uongozi wa hospitali hiyo kumtaka Mhumba kupeleka ushahidi wake katika kikao cha mwisho cha kamati ya nidhamu kitakachokutana Mei 26 kujadili suala hilo, Dk Mmbando alisema: “Wasiliana na uongozi wa KCMC. Hilo ni suala la kiutawala walishughulikie wao,” alisema Dk Mmbando ambaye aliwahi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Kauli ya Dk Mmbando inaendana na kauli ya Katibu Mkuu wa Tughe Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Msuya ambaye juzi alisema uongozi huo ulitakiwa kukanusha tuhuma badala ya kumtafuta aliyetuma ujumbe.
Hata hivyo, uongozi wa KCMC umeendelea kukaa kimya hata baada ya kupelekewa maswali na gazeti hili kwa maandishi kama ilivyoelekezwa na ofisa uhusiano wa hospitali hiyo.MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni