Idara
ya ujasusi ya Korea Kusini imesema kuwa waziri wa ulinzi wa Korea
Kaskazini ameuawa kwa kutokuwa muaminifu kwa kiongozi wa nchi hiyo,
Kim Jong-un.
Taarifa hiyo iliyotolewa bungeni imesema Hyon
Yong-Chol alikutana na mauti yake baada ya kupigwa kwa kombora la
kuangusha ndege mbele ya mamia ya maafisa wakuu serikalini mwishoni mwa
mwezi Aprili.Bwana Hyon anasemekana kuwa alisinzia katika hafla iliyokuwa ikihutubiwa na rais Kim jambo lililomuudhi sana kiongozi huyo wa kiimla.
Hata hivyo ukweli wa ripoti hiyo haujabainika kutokana na usiri wa serikali ya Korea Kaskazini.
Bwana Hyon alipandishwa cheo na kuwa Generali mwaka wa 2010 na kuuawa kwake kunatia shaka udhabiti wa uongozi wa rai Kim Jong -un.
Hyon alipandishwa cheo na kutangazwa kuwa waziri wa usalama wa taifa mwaka uliopita.
Mwandishi wa BBC aliyeko huko Seoul anasema mauaji hayo ya kikatili mbele ya umma ikiwa yatathibitishwa, yanaonyesha athari za uasi dhidi ya Kim Jong-un.
Mapema idara hiyo ya ujasusi ilisema viongozi wakuu katika serikali ya Korea Kaskazini wamekuwa wakiuawa kwa wastani wa mmoja kwa wiki.
Mara ya mwisho kwa kiongozi huyo wa korea kaskazini kuamrisha kuuawa kwa kiongozi mkuu serikalini ilikuwa ni mwaka wa 2013 alipoamrisha ami wake
Chang Song-thaek - kukamatwa na kutiwa kitanzi.
Chang alikamatwa katika mkutano wa hadhara na kupelekwa katika eneo la hadhara alikouawa mbele ya umma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni