Kifungo cha waliokamatwa wakibusu chaendelezwa na mahakama Tunisia
Mahakama ya rufaa
nchini Tunisia imeamuru kuendelezwa kwa hukumu ya wapenzi wawili waliokamatwa mwezi
Septemba kwa kubusu wakiwa ndani ya gari lao.
Nessim Ouadi, ambaye
ni raia wa Ufaransa pia alilaumiwa kwa kupuuza maagizo ya baada ya
kukamatwa pamoja na mpenzi mwanamke raia wa Tunisia. Wawili hao
walipewa vifungo vidogo ikiwa ni miezi minne kwa mwanamume na miwili kwa
mwanamke tofauti na walivyopewa mwezi Oktoba.
Kesi hiyo ilisababisha malalamiko katika mitandao ya kijamii na
kuzua mjadala nchini Tunisia kuhusu maadili katika maeneo ya umma na
wajibu wa polisi. Mkuu wa mshataka alisema kuwa kesi hiyo
imeripotiwa kwa njia isiyofaa na vyombo vya habari vya kimataifa na kuwa
wawili walikuwa uchi na walikuwa wakifanya mapenzi wakati
walisimamishwa na polisi. Jambo hili linazua mawsali mengi kwa sababu sio rahisi watu kuendesha gari huku wakifanya mapenzi
Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani inaonyesha kuwa
watu takriban milioni moja hujiua kila mwaka. Nini sababu kuu za watu
kujiua, mazingira ya tukio hilo kiakili na nini kifanyike kukabiliana na
majaribio ya kujiua?
Bondia Anthony
Joshua anatarajiwa kutetea mataji yake ya IBF na WBA atakapovaana na
Carlos Takam baada ya Kubrat Pulev kujitoa kufuatia majeraha.
Pambano
hilo linalotarajiwa kuwa kali na la kuvutia litapigwa Oktoba 28 katika
dimba la Cardiff ambapo mpaka sasa tiyari tiketi 70,000 zimeshauzwa.
Litakuwa pambano la kwanza la Joshua tokea alipomtwanga Wladimir Klitschko katika dimba la Wembley April.
Pulev alipata majereha ya bega wakati akijiandaa na mchezo huo.
Takam mzaliwa wa Cameroon na anayeishi nchini Ufaransa ana miaka 36 na anatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa Joshua.
Idadi
kubwa ya waandishi chipukizi nchini Tanzania, wanakabiliwa na
changamoto moja kubwa. Nayo si nyingine isipokuwa ni kushindwa
kufikia ndoto ya kuchapisha walau kitabu kimoja kwa sababu ya
kutokumudu gharama za uchapishaji wa vitabu.
Kuchapisha
kitabu chenye kiwango ( standard ) kinacho hitajika sokoni,
ambacho kinaweza kukubaliwa na wauzaji na wasambazaji wakubwa
nchini, mwandishi anatakiwa kwa kadirio la chini kabisa, awe na
walau kiasi cha shilingi LAKI NANE hadi MILIONI MOJA NA NUSU
kutegemea na ukubwa wa kitabu.
Kiasi
hiki kinaonekana kuwa kikubwa mno kwa mwandishi chipukizi ambae
ndio kwanza anataka kutumia kipaji chake cha uandishi kujipatia
fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yake ya kila siku na
kupata maendeleo kwa ujumla.
Mwisho
wa siku waandishi hawa huamua kukata tamaa ya kutimiza ndoto
yao hiyo adhimu na matokeo yake mawazo waliyo taka kuyaandikia
kitabu hufa ama kupotea.
Serikali ya jimbo
moja nchini Nigeria imempa heshima rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, kwa
kumjengea sanamu kubwa ya shaba na kuipa barabara moja jina lake.
Wakati
akifanya ziara katika jimbo lililopo kusini mashariki la Imo siku ya
Jumamosi na Jumapili, Bw. Zuma alipewa cheo cha kiongozi wa kitamaduni
ambacho ndicho cha juu zaidi kinachotolewa eneo hilo. Muungano wa
mashirika ya kupambana na ufisadi (CSNC) ambao ni wa zaidi ya mashirika
150 ya kupambana na ufisadi nchini Nigeria, umemlaani gavana wa jimbo
Rochas Okorocha, kwa kumtambua Zuma kama mtu shujaa mbele ya kundi la
vijana wa Afrika, wakati anakabiliwa na shutuma nyingi za ufisadi nchini
mwake. "Ni kama Gavana Okorocha hafahamu kuwa watu wa Afrika Kusini kwa
sasa, wanamtaka rais wao ajuzulu kwa kuleta aibu kwenye nchi ya Nelson
Mandela?" uliandika katika taarifa. Pia taarifa hizo zimekosolewa vikali katika mtandao wa twitter.
Kila mtu amekuwa
akidhania kwamba uhusiano wa wapenzi maarufu Afrika Mashariki na kati
msanii wa bongo fleva Diamond Platinumz na mfanyibiashara wa Uganda Zari
Hassan ulikuwa umevunjika baada ya kashfa ya Diamond iliomhusisha na
mwanamitindo Hamisa Mobeto.
Zari yeye mwenyewe amjitokeza na
kushutumu uvumi huo ambao umekuwa ukisambaa katika mitandao ya blogi,
kufuatia hatua yake ya kuondoa picha za Diamond katika mitandao yake
mbali na kutohudhuria sherehe ya kuzaliwa kwake.
Inadaiwa hata kadi ya siku ya kuzaliwa hakumtumia mpenziwe na baba ya watoto wake wawili Diamond Platinumz.
Wakati Diamond alipokiri kuwa na uhusiano mwengine nje ya ndoa na Hamisa
na kupata mtoto naye ilikuwa mwanzo wa vita vya mitandaoni kati ya
wapenzi hao wawili na kuzua uvumi kwamba huenda wataachana.
Hata hivyo
akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu kisa hicho Zari amethibitisha
kwamba bado yuko na mpenziwe Diamond na kile wanachojaribu kufanya ni
kutoweka hadharani maisha yao huku wakiendelea kushauriana.
Alisema:
Nilimtakia siku njema ya kuzaliwa lakini sio hadharani bali katika
mtandao wa Whatsapp.Tunajaribu kuondoa maisha yetu ya kibinafsi katika
mitandao ya kijamii. Na kila tunapoendelea kujiondoa katika mitandao ya
kijamii ndio tunazidi kupata uvumi, lakini hakuna tatizo kama hilo kila
kitu kiko shwari, Zari alisema katika mahijiano na idhaa moja maarufu ya
Tanzania.
Habari za penzi lao kuisha zilizusha madai kwamba hatua
hiyo itaathiri mikataba ya mamilioni ya fedha waliotia saini ikiwemo
kampuni kadhaa.
Umewahi kujaribu
kumuua mbu au nzi kwa mikono? Utagundua kwamba huwa vigumu sana. Wadudu hawa huwa
na kasi ya ajabu. Lakini inakuwaje wadudu hawa wadogo - wenye ubongo mdogo
hivi - wanaweza kuwazidi binadamu kwa urahisi hivi?
Je, huwa wanaweza kujua kwamba unataka kuwaua hata kabla ya kujaribu kuwaua?
Ni swali ambalo watu wengi wamekuwa wakijiuliza, lakini usishangae tena.
Sababu ya wadudu hawa kuwazidi binadamu na wanyama wengine ni mtazamo wao wa dunia.
Wadudu hawa huitazama dunia kwa mwendopole yaani 'slowmotion' ukilinganisha na tunavyoyatazama matukio.
Kwa kufafanua, hebu utazame mshale wa saa.
Kama binadamu, huwa unauona mshale huo wa saa ukienda kwa kasi fulani.
Lakini kwa wanyama wengine hali ni tofauti.
Mfano kasa atautazama ukienda kwa kasi mara mbili zaidi ya kasi anayoiona binadamu.
Kwa
mbu, nzi na wadudu wengine wa karibu, mshale huo wa saa watauona
ukienda kwa kasi mara nne chini ya kasi anayoitazama binadamu.
Kimsingi, kasi ya kuenda kwa wakati hubadilika kutoka kwa mnyama hadi mwingine.
Wanyama kimsingi huutazama ulimwengu kama video inayocheza mfululizo.
Kwa
kufafanua, huwa wanaunganisha picha nyingi kutoka kwenye sehemu zao
nyingi kwenye macho hadi kwenye ubongo kwa kasi ya juu, mara kadhaa kila
sekunde. Kwa binadamu, picha hizi hutumwa mara 60 kila sekunde, kwa kasa
mara 15 kila sekunde, na kwa mbu, nzi na wadudu wengine wanaopaa mara
250 kila sekunde!!!
Tofauti
Kasi
ambayo picha hizi husomwa kwenye ubongo wa mnyama huweza kupimwa. Kwa
kawaida, wanyama wadogo huwa na kiwango cha juu cha kasi hii, ikiwa ni
pamoja na mbu na nzi. Binadamu kwa sababu ni wanyama wakubwa, kiwango
chao cha kasi hii kiko chini.
Prof Roger Hardie, wa chuo cha
Cambridge, amekuwa akitafiti jinsi mbu na nzi hufanya kazi, na ameandaa
hata kipimo cha kupima kiwango hiki cha kasi ya mnyama au mdudu kufasiri
picha kwenye ubongo.
"Kiwango hiki kwa ufafanuzi mwingine ni kasi
ambayo mwanga unafaa kuwashwa na kuzimwa kabla ya kutambuliwa na ubongo
au kuonekana kama mwendelezo wa mwanga," anasema Prof Hardie.
Roger
huweka vipande vidogo vya glasi kwenye sehemu ya macho ambayo huusoma
mwanga na kisha kuwasha taa ya LED kwa kasi na kuendelea kuongeza kasi
hiyo huku akifanya vipimo vyake. Kila taa inapowashwa, nishati fulani
huzalishwa kwenye sehemu hiyo ya jicho inayosoma mwanga na nishati hii
inaweza kupimwa na kompyuta na mchoro kuandaliwa.
Vipimo vyake
vimebaini kwamba nzi wenye uwezo wa kuona kwa kasi zaidi wanaweza
kutenganisha mng'ao wa mwanga mara 400 kwa sekunde.
Uwezo wao ni mara sita zaidi ya uwezo wa binadamu.
Nzi
mwenye uwezo wa juu zaidi hufahamika kama "nzi muuaji". Ni nzi mdogo
sana mla wadudu ambaye hupatikana maeneo ya Ulaya. Huwa anapaa na
kuwanasa nzi wengine wakiwa angani kwa kasi ya juu ajabu.
Kwenye
maabara yake ya "nzi" katika chuo kikuu cha Cambridge, Dkt Paloma
Gonzales-Bellido anadhihirisha uwezo wa juu wa nzi hao wauaji kwa
kumwachilia mdudu mla matunda ndani ya kisanduku maalum ambapo mtu
anaweza kupiga picha. Ndani yake kuna nzi muuaji wa kike.
Paloma ananakili wanachofanya nzi hao kwa kupiga
video ya fremu (picha) 1,000 kwa sekunde kwa kutumia kamera za video za
mwendopole. Nzi anapoanza kusonga, anapiga video ya sekunde 12 na
kuhifadhi video hiyo.
Anatumia njia maalum, ya kuhifadhi video
fupifupi ambazo zinajifuta kila sekunde 12 na kuhifadhi sekunde 12 za
mwisho pekee baada ya kuhakikisha kwamba amenasa tukio.
"Muda wetu
wa kuchukua hatua ni wa mwendopole sana kiasi kwamba iwapo tungebofya
kwa kawaida kwenye kitufe cha kupiga video wakati tunafikiria kwamba
tukio hilo linafanyika, tukio hilo litakuwa lilishafanyika," anasema Dkt
Gonzales-Bellido. Hatuwezo kutumia uwezo wetu pekee kutegemea tutabofya
kitufe nzi wakianza kuchukua hatua.
Vita vya nzi
Nzi
huyo muuaji na windo lake wakiwa ndani ya kisanduku, mwanzoni nzi huyo
muuaji alikaa tu bila kufanya chochote, lakini nzi mla matunda alipopaa
umbali wa sentimeta 7 hivi, ghafla bin vuu, nzi muuaji aliruka na
kufumba na kufumbua macho nzi akawa amegeuzwa kuwa mlo.
Ni baada ya kuangalia video ya mwendo pole kwenye kompyuta ambapo inakuwa wazi nini kilifanyika.
Nzi
huyo muuaji alipaa, akamzunguka nzi huyo mla matunda mara tatu
akijaribu kumnasa, na mwisho akafanikiwa kumkamata kwa miguu yake ya
mbele.
Hayo yote kuanzia kupaa hadi kutua tena na windo lake yalitokea kwa sekunde moja pekee.
Kwa macho yetu, hilo linaonekana kama tukio la ghafla.
Kwa
kweli basi, kitendo chetu cha kujaribu kumnasa au kumuua nzi kwa mkono
basi kwa nzi mkono huonekana ukienda kwa mwendo wa konokono.
Hilo humuwezesha mbu au nzii kupaa na kutoroka kabla ya mkono wako kumfikia.
Ili
kumwezesha nzi huyu muuaji kufikia kasi hii ya ajabu, ambayo inazidi
ya nzi wengine, seli zenye kugundua mwanga kwenye macho ya nzi hao huwa
na mitochondria (betri au kiwanda cha nishati ndani ya seli) kwa kiasi
cha juu kuliko kwenye seli sawa katika nzi wengine.
Hizi ndizo
betri za seli na kwa hivyo basi, jambo ambalo linadokeza kuwa ili kuona
kwa haraka lazima mdudu, mnyama au ndege yoyote yule kuwa na kiasi cha
juu cha nishati kuliko wakati anaona kwa mwendopole.
Hii labda inafafanua ni kwa nini macho yote hayana uwezo sawa.
Kwa sababu nzi muuaji hula nyama, nyama hiyo humpa viwango vya juu vya nishati anayoihitaji kutumia kwenye seli hizo za macho.
Hata
kama tungekuwa na kiasi sawa cha mitochondria kwenye seli za macho
yetu, hatungekuwa na kasi sawa ya kuona sawa na ya nzi hao kwa sababu
muundo wa seli za kutambua mwanga ndani ya macho ya nzi bado huwa
tofauti na wa viumbe wengine wenye uti wa mgongo.
Asili ya hili imo katika asili ya viumbe wenyewe.
Wadudu na viumbe wenye uti wa mgongo walichipuka pamoja.
Wazazi wa makundi haya mawili ya viumbe walitengana karibu miaka 700-750 milioni iliyopita.
Nzi
hutumia viungo vinavyofanana na nyuzi kunasa na kusafirisha mwanga
ndani ya jicho. Viungo hivi huchanganyikana na mwanga lakini si kwa
ndani kama kemikali. Lakini kwenye viumbe wenye uti wa mgongo, huwa na
seli zinazofanana na bomba ndogo ambazo huwa na kemikali kwenye shina
lake ambazo huchanganyikana na mwanga.
Kuna baadhi ya viumbe wenye mti wa mgongo ambao wana uwezo wa kuona kwa kasi kuliko binadamu.
Hili mara nyingi huonekana kuwiana na uwezo wa kiumbe husika kupaa au la, na pia iwapo ni kiumbe mdogo au mkubwa.
Hii huenda ni kwa sababu wanaopaa wanahitaji kuchukua hatua upesi kuepuka kugongana na vitu angani.
Viumbe wenye uwezo wa juu zaidi wa kuona huwa ni wale ambao wanaweza kuwanasa nzi wakiwa angani.
Miongoni
mwa viumbe wenye uti wa mgongo, watafiti katika chuo kikuu cha Uppsala
nchini Sweden waligundua kwamba ndege afahamikaye kama 'pied flycatcher'
ambaye huwanasa nzi wakiwa wanapaa, ana uwezo wa kutambua mwanga
ukiwashwa na kuzimwa mara 146 kwa sekunde.
Uwezo wao wa
kutenganisha mwanga ulikuwa karibu mara mbili zaidi ya uwezo wa
binadamu, lakini uwezo wao haukufikia uwezo wa nzi wa kawaida.
Hii ina maana kwamba ndege, sawa na nzi, hutazama mshale wa saa ukisonga kwa mwendo wa pole zaidi kushinda binadamu.
Inaonekana hii ni kama njia ya kujinusuru kuhakikisha uhai wa viumbe.
Ndege hao wanahitaji kuona kwa kasi ili kuweza kunasa windo, nzi nao wanahitaji kuona kwa kasi kuweza kuwakwepa wanaowawinda.
Utakapojaribu tena kumuua mbu au nzi ushindwe, usife moyo.
Juhudi
zao zinazimwa na mambo ambayo yamekuwepo kutokana na mabadiliko ya
mamilioni ya miaka kwenye viumbe kuhakikisha baadhi ya viumbe
wanaendelea kuishi.
Ndio maana mbu au nzi atauona mkono wako ukielekea upande wake kwa mwendopole na kumwezesha kuukwepa!
Ukivalia viatu vyako bila soksi unajiweka katika hatari ya kupata matatizo makubwa zaidi kuliko kunuka miguu pekee.
Chuo
cha Tiba ya miguu nchini Uingereza kinasema karibuni kumekuwa na
ongezeko la maambukizi ya maradhi yanayosababishwa na kuvu (fangas) kutokana na
kuvuma kwa mtindo wa kuvalia viatu bila soksi, hasa miongoni mwa vijana.
Mtaalamu
Emma Stephenson anasema amekuwa akipokea wanaume wa kati ya miaka 18-25
walio na matatizo kwenye miguu yao ambayo yametokana na kutovalia soksi
au kuvalia viatu visivyowatosha vyema.
Kutovalia soksi siku hivi
kumekuwa mtindo maarufu wa mavazi, na mwanamuziki Sam Smith ni miongoni
mwa watu wanaojitokeza hadharani wakiwa na viatu bila soksi.
Wanaume wengi katika maonesho ya mitindo pia mara nyingi huonesha mavazi wakiwa na viatu bila soksi.
Mwanamuziki
Tinie Tempah amejishindia tuzo nyingi kwa sababu ya mitindo na mara
nyingi katika maonesho ya mitindo ya London huketi viti vya mbele.
Yeye pia huwa mara nyingi havai soksi - lakini anafahamu madhara yake?
"Unyevu
mwingi na joto unaweza kusababisha maambukizi ya maradhi yanayotokana
na kuvu mfano ugonjwa unaosababisha muwasho na kuchubuka kwa ngozi (kwa
Kiingereza athlete's foot)."
Kwa mujibu wa Emma, madhara yake yanaweza kuwa mabaya.
"Moja
ya vitu vibaya nilivyowahi kukumbana navyo ni cha mwanamume mmoja wa
miaka 19 aliyefanya kazi ya kuosha magari. Miguu yake ilikuwa inatokwa
na jasho sana na ilikuwa imechubuka sana."
Lakini bila shaka
itachukua ujasiri kumwambia bingwa wa UFC Conor McGregor kwamba anaweza
kupata matatizo kutokana na mtindo wake wa kuvalia viatu.
Emma anashauri kwamba siri ni kutozidisha, iwapo bado utataka kutovalia soksi.
Jaribu usivae viatu bila soksi kwa muda mrefu.
Jaribu pia kuweka kitu cha kukausha jasho kwenye soli ya kiatu chako kabla ya kukivalia bila soksi.
Kadhalika, kuwa makini kuchunguza miguu yako. Ukigundua unaumwa pahali mwone daktarii upesi.