TIMBWILI! Jamaa mmoja na mkewe ambao wote hawakujulikana majina mara moja wamezua varangati la aina yake mahakamani kisa kikiwa ni kufutiwa kesi na kushindwa kuheshimu amri za maafande.Tukio hilo la aina yake lililoshuhudiwa na mwanahabari wetu lilijiri kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar baada ya mume huyo kufutiwa kesi iliyokuwa ikimkabili ya unyayasaji wa watoto wake wa kuwazaa.
Jamaa huyo na mkewe walizua timbwili hilo wakati mtuhumiwa huyo akitolewa chumba cha mahakama kwenda kuweka sawa nyaraka ili awe huru.
Huku akiwa na hasira, mwanaume huyo alianza kuzozana na polisi huku akiungwa mkono na mkewe wakikataa kutii amri ya askari aliyekuwa akiwaelekeza kwenda chumba kingine ili kukamilisha taratibu za kuwa huru.
Akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Wawili hao walisikika wakitoa maneno makali kuwa wasisukumwe kwani hakimu alikuwa ameshamwachia mwanaume huyo huru, jambo ambalo liliwakera askari na kuwaambia kuwa wanatakiwa kutii sheria na taratibu za mahakama.
Katika sekeseke hilo huku askari wakilazimika kutumia nguvu, jamaa huyo alifanya mgomo baridi akipiga kelele na kufoka hivyo kusababisha watu kushangaa.
Hata hivyo, polisi hao walitumia mbinu ya kuwadhibiti kistaarabu ili kuhakikisha amani inakuwepo mahakamani hapo hivyo mambo yakawa shwari.







