Jumamosi, 28 Januari 2017

Ashtakiwa kwa kuendesha gari akiwa amesimama: Boda boda kazi kwenu!

Ashtakiwa kwa kuendesha gari akiwa amesimama

 Adam Elliott ameshtakiwa kwa kuendesha gari akiwa amesimama
Mtu mrefu ameshtakiwa kwa kuendesha gari akiwa amesimama baada ya kukiri kupeleka gari vibaya.
Adam Elliott alituhumiwa kwa kuwaonyesha madereva wengine kichwa chake kikiwa kinaonekana juu ya paa la gari hilo aina ya Ford Ka.
Elliott mwenye umri wa miaka 26 kutoka mji wa Newcastle, ambaye ana urefu wa mita mbili alikiri kufanya makosa hayo katika mahakama ya Newcastle lakini akalaumu urefu wake.
Akizungumza baada ya kesi hiyo, alisema: Sikuwa nimesimama, mimi ni mrefu ndio maana.
Jaji Robert Adams alisema kuwa ni wazi kwamba Adam alitaka kuonekana akiendesha gari akiwa amesimama ili kuonyesha urefu wake.
''Ilikuwa kitu hatari sana kufanya'',alisema.

APOTEA NJIA NA KUENDESHA BAISKELI KWA SIKU 30

Mwanamume huyo alisimamishwa baada ya kuendesha baiskeli kwa siku 30

Mwanamume mmoja nchini China ambaye alikuwa na matumaini ya kuendesha baiskeli hadi nyumbani kwao kusherehekea mwaka mpya, aligundua baada ya siku 30 kuwa alikuwa amepotea njia.
Mwanamume huyo alikuwa na matumaini ya kuwasil nyumbani kwao huko Qiqihar mkoa wa Heilongjian baada ya kuanzia safari yake huk Rizhao umbali wa kilomita 1,700.
Lakini alisimamishwa na polisi wa trafiki akiwa amepotea umbali wa kilomita 500 katika mkoa wa Anhui.
Wakati waligundua, polisi walimlipia tikiti ya treni ili arudi nyumbani.
Ripoti zinasema kwa mwanamume huyo alikuwa akilala maduka ya intaneti kwa sababu hakuwa na pesa.
Mwanamume huyo hakuwa na uwezo wa kusoma ramani na hivyo alikuwa akitegemea watu kumuelekeza.
Polisi walimsimamisha kwa sababu alikuwa akitumia barabara ambayo baiskeli haziruhisiwi barabarani.
Baada ya kugundua makosa yake, polisi na watu wote waliokuwa kituoni ambapo alisimama walichanga pesa na kumnunulia tikiti ili asafiri nyumbani

WAZAZI WALIOMCHARAZA MWALIMU VIBOKO WASAKWA


MKUU wa Wilaya ya Kalambo iliyopo katika mkoa wa Rukwa, Julieth Binyura ameagiza kusakwa na kukamatwa mara moja wazazi waliomshambulia mwalimu wa Shule ya Msingi Kipanga, Musa Mkalambosa kwa kumcharaza viboko mbele ya wanafunzi wake.
Wazazi hao wenye hasira walimdhalilisha mwalimu huyo kwa kumcharaza fimbo wakimtuhumu kuwaadhibu watoto wao kwa kuwabebesha matofali bila idhini yao ambapo wamemsababishia maumivu makali mwilini. Shule ya Msingi Kipanga iko katika kata ya Samazi mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika wilaya ya Kalambo.
Binyura alilazimika kuitisha kikao kilichowashirikisha wenyeviti wa vijiji , walimu na watendaji waliopo katika katika kata hiyo ambapo aliagiza wote waliotenda uhalifu huo wasakwe, wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria pamoja na kuagiza mwalimu huyo ahamishiwe kwenye shule nyingine wilayani humo.
Alisema mwalimu huyo ana uwezo wa kufanya kazi sehemu yoyote wilayani humo huku akilaani kitendo alichofanyiwa na wazazi ambacho ni cha udhalilishaji huku akiwataka wananchi na wazazi kuachana na tabia ya kuwadhalilisha walimu.
Mashuhuda walidai kuwa wazazi hao wenye hasira wakiwa na fimbo mikononi mwao walifika shuleni hapo hivi karibuni ambapo walimcharaza fimbo mwalimu huyo sehemu mbalimbali za mwili wake huku tukio hilo likishuhudiwa na wanafunzi wake pamoja na walimu wenzake.
Akizungumzia kisa hicho, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Enock Majenga alisema baadhi ya wakazi wakiwemo wazazi walighadhabishwa na uamuzi na mwalimu Mkalambosa kuwaadhibu wanafunzi ambao hawakushiriki kusogeza matofali kwenye eneo ambalo choo cha shule hiyo kinajengwa.
Aliongeza kuwa mwalimu Mkalambosa wakati shule inafungwa aliwaagiza wanafunzi wawe wanafika shuleni hapo kwa ajili ya kusomba matofali na kuyapelekea eneo la ujenzi wa choo cha shule hiyo ambapo baadhi ya wanafunzi walikaidi na kutohudhuria.
Baada ya likizo kumalizika na shule kufunguliwa mwalimu Mkalambosa aliamua kuwaadhibu wanafunzi wote ambao walishindwa kufika shuleni hapo wakati wa likizo ambapo aliwaamuru kusomba matofali na kuyapekeleka kwenye eneo la ujenzi wa choo shuleni hapo.
“Ghafla kundi la wananchi, wengi wao wakiwa wazazi wa wanafunzi hao walifika eneo la shule na kumvamia mwalimu huyo na kuanza kumcharaza fimbo na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake,” alieleza.
Ofisa Elimu wa Kata ya Samazi, Daudi Sengo alikiri kutokea kwa mkasa huo ambapo ameshatoa taarifa wilayani akisisitiza kuwa mwalimu huyo amehamishiwa katika Shule ya Msingi Mbuza iliyopo wilayani humo .

Watu 14 walifukiwa mgodini Geita


Watu 14 wamefukiwa na kifusi juzi katika Mgodi wa Dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya Nyarugusu mkoani Geita, kutokana udongo kuporomoka na kuwaacha watu hao bila mawasiliano na hadi jana kutookolewa mtu yoyote.
Hata hivyo pamoja na sintofahamu hiyo juhudi za uokoaji zinaendelea kwa kasi, huku Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga akisema bado anayo imani kuwa watu hao wataokolewa wakiwa hai.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema moja ya kazi iliyoendelea jana ilikuwa ni kwa vikosi vya uokoaji kuendelea kuchimba kifusi ili kutafuta njia ya kuwafikia waathirika huku mipira zaidi ya Oxygen ikiingizwa chini ya mgodi waliko watu hao ili kuwaongezea hewa.
Watanzania 13 na raia mmoja wa China walifukiwa na kifusi juzi usiku baada ya udongo kukatika na kuziba mlango waliokuwa wakitumia kuingia na kutoka. Mkuu wa Mkoa aliliambia gazeti hili jana kuwa hadi jana walikuwa bado hawajafanikiwa kuwafikia watu hao lakini kazi ya kuwafuata waliko inaendelea kwa kasi.
Akizungumza akiwa eneo la tukio, Kyunga alisema vyombo mbalimbali vya uokoaji kwa kushirikiana na wananchi walikuwa wanaendelea kuchimba kifusi ili kuwasaka mahali walipo mgodini.
“Kutokana na uzoefu wa kazi na matukio kama haya yaliyowahi kutokea tuna matumaini makubwa ya kuwaokoa wakiwa hai kutokana na mlango uliojiziba na udongo na watu hao wako katika mtaro wa mlalo hivyo kwa kutumia Oxygen tunayoingiza kwa mipira tutawakuta wakiwa hai,” alisema.
Kyunga alieleza kuwa watu wengi wapo katika eneo hilo wakiwemo ndugu wa waliofukiwa lakini kwa juhudi wanazoziona za uokoaji wametulia na kufuata maelekezo wanayopewa ikiwemo kukaa mita 500 kutoka eneo la tukio.
Alisema wametakiwa kukaa mbali na eneo hilo la uokoaji ili wasisongamane na watu wanaoendelea na uokoaji ili kuwapa fursa nzuri ya vikosi vyote kujadiliana namna ya kufanywa kwa ajili ya kufanikisha uokoaji huo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjoli alisema juhudi za uokoaji zinaendelea kwa ushirikiano wa vikosi vya uokoaji vya Kampuni ya Geita Gold Mine (GCM), Jeshi la Zimamoto na Polisi pamoja na kikosi cha ukoaji cha Sekta ya Madini. Alisema hali ni shwari katika eneo la tukio na wana matumaini ya kuwafikia watu hao wakiwa hai.
Kampuni inayoendesha mgodi huo imesema kutokana na kitabu cha orodha ya watu wanaojiandikisha kuingia mgodini, kuna majina ya Watanzania 12 na Mchina mmoja waliofukiwa kifusini. Ilielezwa kuwa watu pia waliomshuhudia Mtanzania mmoja akingia mgodini humo bila kujiandikisha na hivyo kufanya waliofukiwa kufikia 14.

DC ALIYEJIUZULU ATUA DAR


*Ikulu yathibitisha
Na AGATHA CHARLES-
DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, amethibitisha kujiuzulu kwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele.
Kupitia taarifa yake iliyoandikwa kwa kifupi na kutumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Msigwa, hakutaja sababu ya Mnyele kuomba kujiuzulu bali alisema: “Ombi la Mnyele aliyeomba kujiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora limekubaliwa na Rais Dk. John Magufuli. Nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora itajazwa baadaye.”
Taarifa hiyo ya Ikulu ilitumwa jioni ya jana wakati asubuhi yake Mnyele alikuwa tayari ameshaondoka katika kituo chake cha kazi cha Uyui na kuja Dar es Salaam.
Gazeti hili lilipata taarifa na baadaye kuthibitishwa na Mnyele mwenyewe kwa njia ya simu kuwa alikuwa yuko safarini akitoka mkoani humo na angefika Dar es Salaam jana jioni akitumia usafiri wa ndege.
Alitoa taarifa hizo alipozungumza na gazeti hili saa tano asubuhi alipokuwa uwanja wa ndege akisubiri kupanda ndege na kumtaka mwandishi amtafute baada ya saa 10 jioni.
“Tayari niko Dar es Salaam nimeshatoka Uyui, huko nitarudi kukabidhi mwenzangu atakapoteuliwa,” alisema Mnyele.
Gazeti moja marufu nchini lilipotaka kujua sababu za kuchukua uamuzi huo, alisema ulikuwa ni uamuzi binafsi na alimweleza Rais Magufuli hivyo hawezi kuutaja hadharani.
“Uamuzi wa mteuliwa na anayeteuwa ni privacy (siri), hizo ni sababu binafsi, mimi au rais hawezi kuweka hadharani,” alisema.

DC ANUSURIKA KIPIGO ATOKA NDUKI

Mkuu wa Wilaya ya Chemba-Dodoma, Simon Odunga akila kiapo 

Sakata hilo ni baada ya DC huyo kuwataka wananchi wasilime mashamba yao kwa madai kuwa eneo hilo la ekari 500 linamilikiwa na mwekezaji. 

Baada ya mkuu huyo kuwatolea lugha chafu na kuamuru mwenyekiti wa kijiji akamatwe wananchi walijawa hasira na kuanza kuushambulia msafara wake. 

DC huyo alilazimika kukimbia baada ya gari lake kupigwa mawe

Pia baadhi ya viongozi wa wilaya akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri walilazimika kuvalishwa hijjab na kutoroka.

Ijumaa, 27 Januari 2017

Aliyenyimwa nafasi ya kuenda chooni kulipwa dola milioni 1.3: Walimu wa TZ mpooo!!

Shule ilimuomba msamaha mwanafunzi na mamayake

Shule moja katika jimbo la California nchini Marekani imeamrishwa kumlipa dola 1.25 mwanafunzi wa zamani ambaye alienda haja ndogo kwenye ndoo baada ya kunyimwa nafasi ya kuenda chooni.
Jaji alitoa uamauzi huo kufuati kesi ambapo shule na mwalimu walishtakiwa kufuatia kisa hicho kilichotokea mwaka 2012.
Shule ilisema kuwa mwalimu hakuwa na nia ya kumkosea heshima mwanafunzi.
Mawakili wa shule walisema kuwa mwalimu alijaribu kutafuta suluhu, kwa kile alichofikiri kuwa sheria kali za wanafunzi kutopewa ruhusa ya kuenda chooni wakati wa masomo.
Mwanafunzi huyo wa shule ya Patrick Henry High School, ambaye sasa ana umri wa miaka 19, anasema kuwa mwalimu Gonja Wolf alikataa ombi lake la kutaka kuruhusiwa kuenda chooni.
Bi Wolf badala yake, alimuamuru mwanafunzi kutumia chumba kilichokuwa kando ambapo alikojoa kwa ndoo.
"Kisa kama hiki kamwe hakingefanyika kwa mwanafunzi wa umri wa miaka 14 ambaye alikuwa amejiunga na shule ya sekondani," wakili wa mwanafunzi alisema.
Kando na dola milioni 1.25, jaji pia aliamrisha mwanafunzi huyo kulipwa dola 41,000 kwa huduma za matibabu.
Mwalimu alipewa likizo na hakurudi shuleni humo baada ya kisa hicho.
Shule ilimuomba msamaha mwanafunzi na mamayake na kuwaeleza walimu kuwa nafasi za kuenda chooni zimeruhusiwa.

Albright asema ''yuko tayari kuingia usajili ya Waislamu''

Madeleine Albright asema atajisajili kuwa Muislamu iwapo Trump ataanzisha sajili ya Waislamu Marekani

  Madeleine Albright asema atajisajili kuwa Muislamu iwapo Trump ataanzisha usajili wa Waislamu Marekani
Aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani na msanii wa Bing bang wameapa kujisajili kama Waislamu iwapo Donald Trump ataanzisha sajili ya waislamu pekee.
Mwanasiasa Madeleine Albright na Mayim Bialik walisema kuwa wako tayari kujisajili kuwa wafuasi wa dini hiyo ili kupinga hatua hiyo ya Trump.
''Nililewa kama Mkatoliki , nikawa Episcopalian na baadaye nikabaini kwamba familia yangu ilikuwa ya Kiyahudi'', Bi Albright, ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani alisema katika mtandao wake wa Twitter.
Chapisho hilo lilipendwa na maelfu ya watu.
Tamko lake lilijiri huku kukiwa na uvumi kuhusu agizo la rais ambalo litafanya ukaguzi wa kina, kupiga marufuku wakimbizi mbali na watu wanaoingia kutoka nchini humo kutoka mataifa saba ambayo yatashirikisha Syria,Yemen na Iraq.
Lakini hakujakuwa na usajili wa Wamarekani Waislamu katika miezi ya hivi karibuni, swala ambalo bwana Trump alisema atalitekeleza katika mahojiano mwaka 2015 kabla ya kukana kufanya hivyo.

SIRI NZITO DC KUJIUZULU


Na Mwandishi Wetu, Tabora
MKUU wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele, amejiuzulu wadhifa wake, huku akiwa na siri nzito.
Mnyele ambaye kitaaluma ni mwanasheria msomi, amejiuzulu jana huku akiwa amedumu katika wadhifa huo kwa miezi minane tangu ateuliwe na Rais Dk. John Magufuli.
Hata hivyo hakuweka wazi sababu za kujiuzulu kwake.
Taarifa zinaeleza kuwa, jana Mnyele alikutana na Kamati ya Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuwaaga rasmi kuwa yeye si mtumishi tena wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Said Ntahoni ambaye alihudhuria kikao cha madiwani wa Wilaya ya Uyui, alikiri kujiuzulu kwa Mnyele na kusema ameacha pengo kubwa katika wilaya hiyo.
“Ni kweli amejiuzulu nafasi hii tangu jana, amekuja mbele ya Kamati ya Madiwani CCM Wilaya, akatwambia amejiuzulu nafasi yake, japo hakuweka wazi sababu za kuchukua uamuzi huo.
“Aliwaambia wajumbe kwamba amemwandikia barua Rais Magufuli na ameridhia aachie ngazi…wajumbe wengi walibaki wameduwaa kwa sababu yeye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya yetu… kwa kuwa ni uamuzi wake hatukuwa na namna tena.
“Tumekuwa naye kwa miezi nane hapa, ametusaidia katika mambo mengi, nguvu yake ilikuwa bado inahitajika kwa wanaUyui ambao amekuwa akifanya nao kazi za kila siku,” alisema Ntahoni.
Alisema pengo la Mnyele ni kubwa, lakini anaamini Rais Magufuli atawapelekea kiongozi mwingine mchapakazi ambaye watashirikiana nae kwa kila nyanja ili kuinua maendeleo ya wilaya hiyo.
MNYELE
MTANZANIA ilimtafuta DC Mnyele na alipoulizwa iwapo amejiuzulu nafasi yake, alianza kwa kusema. “Ndo nasikia kwako niko ofisini kwangu naendelea kuchapa kazi niliyotumwa na mamlaka za uteuzi.
“…unajua unapoteuliwa unatangazwa, unapotumbuliwa unatangazwa sasa taarifa hizo wewe umezitoa wapi?
“Ukitaka kujua suala hili, sehemu nzuri na ‘source’ wa uhakika mtafute Gerson Msigwa (Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu), anajua ‘issue’ (suala) hili,” alisema Mnyele.
Hata hivyo Msigwa alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema hajapata taarifa zozote kutoka mamlaka zinazohusika juu ya kiongozi huyo kujiuzulu.
Wakati ikiwa haijulikani sababu za kujiuzulu kwake, taarifa nyingine zinasema Mnyele amefikia uamuzi huo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na kutingwa na majukumu yake binafsi aliyonayo.
Chanzo chetu cha uhakika, kinasema Mnyele aliandika barua ya kuomba kijiuzulu mwaka jana, kwa Rais Magufuli ambayo ombi lake limekubaliwa na amejibiwa juzi.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao, waliiambia MTANZANIA kuwa jana asubuhi Mnyele alipita kila idara akianzia ofisini kwake kuaga wafanyakazi, huku akionekana kuwa ni mwenye furaha.
“Bosi wetu alianzia ofisini kwake kuaga watumishi, baadae alipita kila idara na kubwa ambalo alikuwa akieleza ni uamuzi ambao ameufanya yeye mwenyewe bila shinikizo.
“Bosi wetu kasema uamuzi wa kusitisha ajira yake hautokani na kushindwa kwendana na kasi ya Rais Dk. Magufuli, bali anataka kufanya kazi zake
binafsi,” alisema mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo (DED), Hadija Makuwani alisema yeye ni miongozi mwa watu walioagwa jana asubuhi na mkuu huyo wa wilaya.
Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ili kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa kutokana na kuwa wilayani Nzega kwa shughuli ya ukaguzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.
CHANZO MTANZANIA

Al-Shabab washambulia kambi ya jeshi la Kenya nchini Somalia

Wapiganaji wa al-Shabab

Al-Shabab wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa
Kundi la al-Shabab nchini Somalia limesema wapiganaji wake wameshambulia kambi ya jeshi la Kenya chini ya kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom) nchini Somalia.
Wapiganaji hao wanadai kuwaua wanajeshi wengi kwenye shambulio hilo katika kambi ya Kulbiyow kusini mwa Somalia karibu na mpaka wa nchi hiyo na Kenya.
"Mujahideen (wapiganaji) wawili walivurumisha magari yaliyokuwa na mabomu na kuyalipua kwenye lango la kambi hiyo ya mji wa Kulbiyow kabla ya wapiganaji wengine kuingia. Baada ya mapigano makali, tumefanikiwa kuiteka kambi," mmoja wa wasemaji wa al-Shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab ameliambia shirika la habari la Reuters.
Msemaji huyo amedai kundi hilo limewaua wanajeshi zaidi ya 50 na kutwaa magari na silaha za wanajeshi hao, taarifa ambazo msemaji wa majeshi ya Kenya amekanusha.

Naye Kanali Paul Njuguna ameiambia Reuters: "Ni uongo. Operesheni ya kijeshi inaendelea. Tunaendelea kupokea taarifa."

Al-Shabab wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Somalia inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi na jamii ya kimataifa.
Wanajeshi wa Kenya pamoja na wanajeshi kutoka Djibouti, Uganda na Ethiopia, chini ya Amisom, wamekuwa wakisaidia serikali hiyo yenye makao yake mjini Mogadishu.

Januari mwaka uliopita, wapiganaji wa al-Shabab walishambulia kambi yajeshi la Kenya ya el-Adde na kuua wanajeshi wengi.
Al-Shabab walisema waliua zaidi ya wanajeshi 100. Jeshi la Kenya halijatangaza idadi kamili ya wanajeshi waliouawa hadi wa leo.